Iran imeripotiwa kuishambulia meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Thailand iliyokuwa ikijaribu kupita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz ( Straight Hormuz), na hivyo kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo ambalo tayari ni tete la Ghuba.
Kulingana na ripoti za vyombo vya baharini na usalama, meli ya kubeba mizigo iliyosajiliwa Thailand Mayuree Naree ilipigwa na makombora ilipokuwa ikisafiri takriban maili 11 kaskazini mwa Oman. Shambulio hilo lilizua moto ndani ya meli na kuwalazimu wahudumu kuacha meli. Takriban wafanyakazi 20 waliokolewa, huku wengine kadhaa wakiripotiwa kutoweka, kwa mujibu wa mamlaka ya Thailand.
Meli ya Thailand haikuwa meli pekee iliyolengwa. Angalau meli tatu za kibiashara zilipigwa katika matukio tofauti katika Mlango-Bahari wa Hormuz siku ya Jumatano, zikiangazia hatari inayoongezeka kwa njia za meli za kimataifa.
Shambulio hilo linakuja huku kukiwa na makabiliano makubwa zaidi ya kijeshi yaliyohusisha Iran na vikosi vya Magharibi, ambayo tayari yamesababisha vitisho vya mara kwa mara dhidi ya meli zinazotumia njia ya kimkakati ya majini. Mlango wa bahari wa Hormuz ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za baharini duniani, hubeba takriban 20% ya usafirishaji wa mafuta duniani, kumaanisha usumbufu wowote unaweza kuwa na madhara makubwa kwa masoko ya nishati ya kimataifa.
Mlango wa bahari wa Hormuz hubeba karibu 20% ya usambazaji wa mafuta ulimwenguni. Shambulio lolote dhidi ya meli za kibiashara hapa sio suala la kikanda tu, linaweza kuwa mzozo wa kiuchumi wa ulimwengu haraka.

