Baada ya kifo cha Mtume Muhammad (SAW) mwaka 632 BK, Waislamu walikabiliwa na swali moja kubwa:

 


 nani angeongoza jamii ya Kiislamu baada yake? Sehemu kubwa ya Masahaba walikusanyika na kumchagua Abu Bakr (RA) kuwa khalifa wa kwanza. Waliona uongozi wa Waislamu kuwa jambo la mashauriano ya jamii (shura). 

Hata hivyo, kundi jingine lilikuwa na mtazamo tofauti. Wao waliamini kuwa Mtume tayari alikuwa ameonyesha wazi kwamba binamu yake na mkwe wake Ali ibn Abi Talib ndiye aliyestahili kumrithi. Kundi hili lilijulikana kama Shīʿat ʿAlī, yaani “wafuasi wa Ali.” Ndipo chanzo cha jina Shia kilipoanzia.


Kwa muda fulani mgawanyiko huo haukuonekana wazi sana, kwa sababu Ali aliendelea kuwa sehemu ya uongozi wa Kiislamu. Lakini hali ilianza kubadilika baada ya kipindi cha makhalifa watatu wa kwanza. Baada ya kuuawa kwa khalifa wa tatu Uthman ibn Affan mwaka 656, Ali alichaguliwa kuwa khalifa wa nne. Hata hivyo, uongozi wake uliingia katika kipindi cha migogoro mikubwa ya kisiasa na vita vya ndani vilivyojulikana kama Fitna ya Kwanza. Moja ya migogoro mikubwa ilikuwa kati yake na gavana wa Syria Muawiya I, iliyosababisha Battle of Siffin. Hatimaye Ali aliuawa mwaka 661 na kundi la Kharijites, jambo lililofungua njia kwa Muawiya kuanzisha nasaba ya Umayyad.


Lakini tukio lililobadilisha kabisa historia ya Shia lilitokea miaka michache baadaye. Mwaka 680, mwana wa Ali, Husayn ibn Ali, alisimama kupinga utawala wa Yazid I. Safari yake ilimalizika kwa tukio la kusikitisha sana katika Battle of Karbala, ambapo yeye pamoja na wafuasi wachache waliuawa. 

Hivyo Kwa Shia, Karbala si tukio la kihistoria tu bali ni ishara ya milele ya kusimama dhidi ya dhuluma. Ndiyo sababu kila mwaka siku ya Ashura wanaikumbuka kwa maombolezo na ibada zao ambazo wao huzifanya.


Katika karne zilizofuata, wafuasi wa Shia waliendelea kuendeleza mafundisho yao kuhusu uongozi wa kiroho unaoitwa Imamah. Walisisitiza kwamba viongozi wa kweli wa Kiislamu wanapaswa kutoka katika familia ya Mtume, Ahlul Bayt. Baadaye, ndani ya Shia yenyewe kulizuka migawanyiko. Wapo wanaoitwa Twelvers, ambao wanaamini katika mlolongo wa Maimamu kumi na wawili na wanangoja kurudi kwa Imamu wa mwisho, Muhammad al-Mahdi. 

Kuna pia Ismailiya na Zaidiya, kila kundi likiwa na tafsiri yake kuhusu urithi wa Imamu.


Kwa karne nyingi Shia walikuwa wachache na mara nyingi walipata shinikizo chini ya tawala za Sunni kama Umayyad na Abbasid. Hata hivyo, historia ilibadilika sana mwanzoni mwa karne ya 16 wakati nasaba ya Safavid ilipoibuka katika eneo la Iran. Kiongozi wao, Shah Ismail I, aliteka mamlaka mwaka 1501 na kuanzisha dola ya Safavid. Hapa ndipo tukio kubwa lilipotokea: alitangaza madhehebu ya Shia Ithna Ashariya kuwa dini rasmi ya Iran.


Sababu za hatua hiyo zilikuwa za kidini lakini pia za kisiasa. Wakati huo, eneo kubwa la ulimwengu wa Kiislamu lilikuwa chini ya Dola ya Ottoman, ambayo ilikuwa Sunni. Safavid walitaka kujenga utambulisho tofauti na wa kipekee ili kuimarisha mamlaka yao na kuzuia ushawishi wa Ottoman. Kwa kufanya Shia kuwa dini rasmi, Iran ilijitenga wazi kidini na kisiasa na Dola ya Ottoman. Mgogoro kati ya dola hizi mbili ulipelekea vita vingi kwa karne kadhaa, na mgawanyiko wa Sunni na Shia ukapata sura ya kisiasa na ya kijiografia pia.


Tangu kipindi hicho, Iran imeendelea kuwa kituo kikuu cha Shia duniani. Katika karne ya 20, tukio lingine kubwa lilitokea wakati wa Iranian Revolution, ambapo mwanazuoni wa Kiislamu Ruhollah Khomeini aliiongoza Iran kuwa Jamhuri ya Kiislamu inayotegemea mafundisho ya Shia. 

Tangu hapo, Iran imekuwa moja ya nchi zenye ushawishi mkubwa katika siasa na fikra za Shia duniani.


Leo, Shia wanakadiriwa kuwa takriban asilimia 10 hadi 15 ya Waislamu wote duniani. Wengi wao wanaishi Iran, Iraq, Azerbaijan na Bahrain, huku pia wakiwa na uwepo mkubwa Lebanon na Yemen.

Naaam hiyo ndo historia fupi kuhusu Shia