Waziri Mkuu Ampa Zawadi Ya Laptop Ya Milionin 1.9 Mwanafunzi Wa Shule Ya Kata
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema shule za sekondari za kata zina fursa ya kufanya vizuri kama zilivyo shule nyingine licha ya kuwa watu wengi wamekuwa wakizidharau. Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatatu, Machi 7, 2016) wakati akikabidhi zawadi ya kompyuta mpakato (laptop) kwa mwanafunzi aliyeshinda shindano la kuandika insha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC ). Kompyuta hiyo ina thamani ya sh. 1,992,000/-. Mwanafunzi huyo, Jabir Mandando (20), amehitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mbekenyera iliyoko wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Amepata ufaulu wa daraja la pili na sasa anasubiri matokeo ya kujiunga na kidato cha tano. Lakini aliandika insha hiyo mwaka jana wakati akiwa kidato cha nne. “Huyu ni mtoto wa kijijini tu. Anatoka kijiji cha Namilema wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi. Shule ya Mbekenyera aliyosoma ni shule ya kata. Ameweza kushinda tuzo na kushika nafasi ya tatu katika shindano lililoshirikisha shule nyingi za Jumuiya ...