Mganga Mbaroni Akidaiwa Kugoma Kumhudumia Mjamzito
Polisi mkoani Mara inamshikilia mganga wa zahanati katika Kijiji cha Rwamchanga wilayani hapa kwa madai ya kushindwa kumhudumia mjamzito aliyejifungua mapacha na kusababisha kifo mtoto mmoja. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’anzi amesema tukio hilo lilitokea Mei 15. “Tunamshikilia kwa makosa matatu, likiwamo la uzembe, kufanya makusudi na kushindwa kuwajibika sawa na kiapo cha kazi yake, tunaendelea na mahojiano yatakapokamilika atafikishwa mahakamani,” amesema Ng’anzi. Akisimulia chanzo cha mwanae kupoteza maisha, Shida Mugesi akiwa katika Hospitali ya Nyerere alisema alifika hospitalini saa 12 asubuhi na kumuomba mganga amuhudumie, lakini alikataa. “Nilikaa kwa muda wa saa mbili bila kupatiwa huduma, ghafla nilihisi uchungu wa kusukuma mtoto tukamuita mganga wa zamu ili anisaidie aligoma na kudai nimsubiri anakwenda kuoga na wakati huo alikuwa anazungumza kwa simu bila kuonyesha ushirikiano. Baada ya kugoma kunisaidia nilianza kujifungua ...