Ikulu Yavunja Ukimya Sakata la Umeya Dar
Ikulu imevunja ukimya kuhusu ile sinema ya kuahirishwa mfululizo kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kusema haitaona tatizo lolote iwapo Halmashauri hiyo itaongozwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Uchaguzi huo utakapofanyika na vyama hivyo kushinda na kuongoza Jiji, Ikulu imesema, hakutaathiri hata kidogo shughuli zake za kila siku hivyo haina mkono wake kwenye sarakasi za uchaguzi huo. Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, alipoulizwa ni kwanini Ikulu isiingilie kati na kuamuru kufanyika kwa uchaguzi huo ambao umeshapigwa danadana muda mrefu. “Hilo la hisia kwamba Ikulu ina mkono wake kwa kuhofia Ikulu kuwa chini ya Ukawa si kweli hata kidogo,” alisema Balozi Sefue. "Sisi tuogope nini wakati wao hawataathiri shughuli zetu za kila siku? Nakuhakikishia hatuoni tatizo lolote." Kumekuwa na tetesi kwamba serikali inahofia upinzani kuchukua Jiji, kwani Ikulu ni kama itakuwa ndani ya eneo linalota...