Wafanyakazi 8,000 Hawajawasilishiwa Michango ya NSSF
Wafanyakazi takriban 8,000 ambao ni wanachama wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) hawajawasilishiwa michango kutoka kwa waajiri wao yenye thamani ya Sh bilioni 21.4. Kutokana na hali hiyo, NSSF imetoa muda wa miezi miwili kwa waajiri wote nchini ambao hawajawasilisha fedha za michango hiyo kwa shirika hilo, kuwasilisha mara michango hiyo kabla ya Julai mosi, mwaka huu. Kwa mujibu wa shirika hilo, endapo muajiri yeyote atashindwa kutekeleza agizo hilo katika muda huo uliotolewa, NSSF haitakuwa na njia nyingine zaidi ya kuwaburuza waajiri hao mahakamani kwa mujibu wa sheria. Aidha shirika hilo, lilibainisha wazi kati ya waajiri sugu wasiowasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi wao kwa shirika hilo, ni Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) na baadhi ya kampuni za ulinzi. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa NSSF, James Aigo alisema ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya NSSF kwa mwajiri kutowasilisha mich...