Aliyezushiwa ujambazi mitandaoni aibuka
Mfanyabiashara wa mjini Arusha aliyetangazwa kupitia mitandao ya kijamii akihusishwa na ujambazi uliotokea Mbagala jijini Dar es Salaam, ameibuka na kukana taarifa hizo na kusema zilisambazwa na washindani wake. Tukio la majambazi kupora na kuua katika benki ya Access tawi la Mbagala lilitokea Februari 26, mwaka huu na watu kadhaa wanaendelea kushikiliwa na polisi. Mfanyabiashara huyo, Ashaeri Mollel aliiambia Nipashe kuwa baada ya tukio hilo, washindani wake ambao hata hivyo hakuwataja, waliisambaza picha yake kwenye mitandao ya kijamii wakimhusisha na tukio hilo, hali iliyomsababishia usumbufu kwa familia na marafiki zake. “Nimekuwa nikipigiwa simu na watu mbalimbali wakiniulizia imekuwaje nikahusika kwenye tukio hilo, sasa inakuwa usumbufu mkubwa na wapo walioathirika kisaikolojia kutokana na uzushi huo,” alisema. Hata hivyo, Mollel alisema katika siku za karibuni alitofautiana na mfanyabiashara mwenzake (jina tunalo) wakati wakiuziana gari, hali iliyosababisha polis...