Magufuli: Serikali Itakomesha Watumishi na Wanafunzi Hewa
RAIS John Magufuli (pichani) amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kumaliza makosa yote yaliyojitokeza huko nyuma ikiwemo tatizo la watumishi na wanafunzi hewa lililoibuka hivi karibuni. Amewataka Watanzania kuacha kuingiza siasa kwenye makosa yanapojitokeza, hasa yale yanayogusa sehemu nyeti kama elimu, kwani yakiachwa kuna uwezekano wa kutengeneza taifa la watu wa ajabu. Alisema tangu aingie madarakani amekumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo matatizo ya rushwa, ukwepaji kodi, watumishi hewa na sasa amekumbana na tatizo la wanafunzi hewa. “Nchi yetu ina changamoto na mambo mengi sana hata mimi nimekumbana na changamoto naziona mwenyewe, nikigeuka hivi watumishi hewa ambao hadi sasa wamefikia 10,500, nikigeuka hivi kuna wanafunzi hewa,” alisisitiza. Alisema ni Tanzania pekee ambayo mtu anaweza kupata daraja la nne kidato cha nne katika elimu ya sekondari, halafu akapata fursa ya kujiunga na chuo kikuu na kupatiwa mkopo wa serikali, wakati mhitimu aliy...