TUCTA Yapinga Mpango wa Rais Magufuli Kukata Mishahara ya Watumishi wa Umma Kutoka Milioni 40 hadi 15 Kwa Mwezi
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) limepinga mpango wa Rais John Magufuli wa kukata malipo ya mishahara ya watumishi wa umma kutoka Sh40 milioni kwa mwezi hadi Sh15 milioni. Akizungumza na viongozi wa vyama vya wafanyakazi Kanda ya Ziwa jijini Mwanza jana, Naibu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya alisema uamuzi huo ni kinyume na sheria na utaligharimu Taifa iwapo wahusika wataamua kwenda mahakamani kupinga mishahara yao kupunguzwa. “Watendaji hawa hawakujipangia mishahara wao wenyewe, bali malipo haya yalipangwa na bodi za mashirika na taasisi husika ambazo kisheria zimepewa mamlaka hayo. Malipo haya hayawezi kupunguzwa kwa kauli za kisiasa bila kuzingatia mahitaji ya kisheria,” alisema. “Iwapo Serikali itatekeleza lengo hili bila kuwapo mjadala mpana na makubaliano ya kisheria kati ya wahusika, basi ijiandae kulipa mamilioni ya fedha kama fidia iwapo watakaokatwa mishahara yao watakwenda mahakamani.” Akiwa mjini Chato wakati wa ...