PROFESA MUHONGO AICHANA MIKATABA YA IPTL, SONGAS NA AGRECO .... ASEMA HAINA TIJA KWA TAIFA
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mikataba yote ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni za kufua umeme siyo mizuri na haina manufaa yoyote kwa Taifa. Profesa Muhongo alisema hayo juzi wakati akijibu hoja ya kuongezeka kwa deni la Tanesco iliyotolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika wizara hiyo, John Mnyika. Kambi ya upinzani imekuwa ikisema mikataba ya Tanesco haina tija kwa Taifa na imekuwa ikiliua shirika hilo. Katika hotuba yake, Mnyika alisema Tanesco imekuwa ikiilipa IPTL Sh300 milioni kwa siku kama gharama za uendeshaji. Profesa Muhongo alikiri kwamba ni kweli deni la Tanesco ni kubwa na limesababishwa na uongozi dhaifu, rushwa, wizi na mikataba mibovu ambayo Tanesco imeingia. Alisisitiza kwamba hakuna mkataba unaolinufaisha Taifa. “Lazima niseme ukweli, mikataba yote ya Tanesco siyo mizuri. Tumekuwa tukiwalipa Songas gharama za uendeshaji Dola 4.6 milioni; IPTL tunawalipa Dola 2.6 milioni; Agreco tunawalipa Dola 2.0 milioni...