Chadema wabeza utumbuaji majipu wa Magufuli, wadai bora Kikwete
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Vincent Mashinji ameponda mtindo wa utawala wa Rais John Magufuli wa utumbuaji wa majipu akisema umekosa dira na kinachoendelea ni utashi wa kisiasa na kukurupuka. Kazi kubwa aliyoifanya Rais Magufuli tangu aingie madarakani, katika kipindi cha miezi sita sasa ni kubana matumizi ya fedha za umma kwa kufuta safari za nje za watumishi, kuzuia mikutano kufanyika mahotelini, kuhimiza mamlaka husika kukusanya kodi, kupambana na watumishi hewa, kuwasimamisha au kutengua uteuzi wa watendaji aliodai kuwa ni wazembe na walioshindwa kwenda na kasi yake pamoja na kuwashughulikia wala rushwa na wahujumu uchumi. Katika namna inayoonekana ni kufuata upepo wa kisiasa, Rais Magufuli huwatumbua baadhi ya watendaji kwenye mikutano ya hadhara. “Kuna vitu vingi vinafanyika lakini hatujui kipi ni kipi na wapi tunaelekea. Kuna mambo mengi yanafanyika, lakini hakuna hata mtu mmoja katika nchi hii anayejua Taifa hili lina mpango gani na l...