Fastjet Yatakiwa Kumlipa Abiria Fidia ya Tsh Milioni 30, Ipo Hapa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeiamuru Kampuni ya Ndege ya Fastjet kumlipa abiria wake, John Mhozya fidia ya Sh30 milioni baada ya kushindwa kumtaarifu kuhusu kuahirishwa kwa safari yake. Mbali na fidia hiyo ya hasara ya jumla aliyoipata abiria huyo kutokana na safari hiyo kufutwa, pia Mahakama hiyo imeiamuru kampuni hiyo kumrejeshea abiria huyo nauli yake ya Sh43,000 alizokuwa ameshalipa na Sh339,000 alizozitumia kwa nauli baada ya kutafuta usafiri mbadala kutoka shirika jingine la ndege. Uamuzi huo ulitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu Kisutu, Respicius Mwijage baada ya kuridhishwa na madai ya abiria huyo katika kesi aliyoifungua mahakamani hapo ya kampuni hiyo kuvunja mkataba. Katika kesi hiyo ya madai namba 4 ya mwaka 2013, Mhozya ambaye pia ni wakili wa kujitegemea wa Mahakama Kuu, alikuwa akiiomba Mahakama iiamuru Fastjet imlipe Sh50,000,000, ikiwa ni hasara ya jumla aliyoipata pia imrejeshee fedha zake za nauli alizokuwa ameshalipa kwa mdaiwa pamoja na nauli aliyotumia kwa...