Symbion Tanzania, Tanesco Zabaruzwa Kortini Zikidaiwa Bilioni 560
Kampuni kutoka Falme za Kiarabu, Rental Solutions and Services LLC imeiburuza mahakamani kampuni ya kufua umeme ya Symbion Tanzania Limited, ikidai kulipwa Dola za Marekani 228,070,655.67 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 560 kama fidia na malipo ya ukodishaji wa mitambo ya kuzalishia umeme nchini. Kesi hiyo Namba 234 ya mwaka 2016 imefunguliwa katika Mahakama Kuu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita. Mdaiwa wa pili katika shauri hilo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo limeunganishwa katika kesi hiyo kama mdau mkuu kwenye sakata hilo ambapo maamuzi yatakayotolewa na mahakama yanaweza kuiathiri. Katika hati ya madai, Kampuni ya Rental Solutions and Services inadai Symbion Dola za Marekani 28,070,655.67 kama malimbikizo ya gharama za ukodishwaji wa mitambo, ambayo hadi sasa Symbion imeshindwa kulipa na pia katika shauri hilo Symbion itatakiwa kulipa Dola za Marekani milioni 200 ambazo ni fidia kwa kampuni hiyo kula hasara kutokana na Symbion kuvunja masharti ya mka...