MZEE WA MIAKA 124 ATOA SIRI YA KUISHI MIAKA MINGI.
MTU aliyeshiriki Mapinduzi ya Zanzibar akikadiriwa kuwa na umri wa miaka 70, Machano Mjomba Machano amezungumza na gazeti hili kuhusu siri ya umri wake na alivyoshiriki kwenye mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika 1964. Mzee huyu ambaye familia yake inamkadiria kuwa na umri wa zaidi ya miaka 124, anaishi Gamba Mabatini, kilometa 25 kutoka Bandari ya Unguja, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Machano ambaye anamshukuru Mungu kwa umri alionao, alisema alikuwa miongoni mwa walioshiriki katika kumlinda Rais Sheikh Abeid Amani Karume wakati alipotangaza mapinduzi hayo redioni , eneo la Rahaleo. Pamoja na masuala mengine, alisema walifanikisha mapinduzi hayo kutokana na kushikamana na kuwa na usiri mkubwa. Aidha alisema kwamba John Okello; aliyekuwa raia wa Uganda, alitumika kuwapa mafunzo ya kazi. Mzee Machano ambaye ameona vizazi vingi vilivyokuja na kupita, inaelezwa kuwa hakuna mtu anayejua umri wake kwa usahihi. Hata yeye anasema aliambiw...