TCRA Yatoa Onyo Kwa Wafanyabiashara Wanaobadili IMEI za Simu FEKI ili Kuwahadaa Wananchi
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa wafanyabiashara wa vifaa vya mawasiliano, kuacha kuwahadaa wananchi kwa kutoa punguzo ili kuwashawishi kununua simu bandia na kutishia kuwafunga miaka 10 jela, faini ya Sh30 milioni au vyote kwa pamoja watakaobainika. Hatua hiyo imekuja wakati mamlaka hiyo ikiwa katika hatua ya kutekeleza mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi, huku ikitarajia kuzima simu feki ifikapo Juni 16. Akizungumza na vyombo vya habari jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Mhandisi James Kiraba alisema kuna wafanyabiashara wajanja wanaobadilisha namba za utambulisho za vifaa vya elektroniki (IMEI) ili kuwahadaa wateja kuwa simu zao siyo feki. Kwa ujanja huo, namba ya utambulisho inakuwa inatumika na simu zaidi ya moja na kutambulika na mfumo licha ya kuwa ni feki. Pamoja na kuonekana ni halisi kwa kipindi wanachozinunua, alisema simu hizo zinazobadilishwa IMEI nazo zitazimwa Juni 16 kwa kuwa ni feki. ...