Maalim Seif Sharif Hamad Aitwa Polisi Kuhojiwa
Jeshi la Polisi Zanzibar litamhoji Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Ijumaa ya wiki hii kuhusu masuala mbalimbali ambayo hata hivyo, hayakuwekwa wazi. Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema jana:“Natambua kuwa wasaidizi wangu watazungumza naye Ijumaa. Wao ndiyo wanajua watamhoji nini.” Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi naye hakuweka wazi badala yake alisema kuna masuala mengi ambayo ofisi yake inahitaji kuyafahamu kutoka kwa Maalim Seif. Hii ni mara ya kwanza kwa Maalim Seif kuhojiwa na polisi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ambao kwa Zanzibar ulirejewa Machi 20, baada ya ule wa Oktoba 25 mwaka jana kufutwa. Maalim Seif ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alipinga kurudiwa kwa uchaguzi huo msimamo ambao pia ulichukuliwa na chama chake. Kiongozi huyo amekuwa akitoa matamko kadhaa ya kuwashawishi wananchi kupinga utawala wa Serikali ...