Zitto Kabwe: Magufuli Hajagusa KANSA Ya Ufisadi
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemtaka Rais John Magufuli kukabiliana na vikundi vya mafisadi vinavyoiba mabilioni ya fedha za umma kupitia mikataba mibovu waliyoingia badala ya kuishia kutumbua majipu. Akizungumza katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake jana, Zitto alisema ACT Wazalendo inaunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kupambana na ufisadi, lakini bado hajagusa kiini chenyewe. Zitto alitolea mfano wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kuwa bado kuna kampuni inayolipwa Sh8 bilioni kila mwezi kwa ajili ya mitambo yake ya umeme. Pia, alisema kashfa ya hati fungani imeongeza deni la Taifa kwa Sh1.2 trilioni. “Bado huo mtambo upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali inawalipa Sh8 bilioni wazalishe au wasizalishe umeme. Hivi ndivyo vikundi masilahi katika sekta ya nishati. Bila kuvibomoa, Rais ataonekana anachagua watu katika vita hii,” alisema Zitto. ...