Rais Magufuli Aokoa Asilimia 4 ya Bajeti
Ndani ya miezi sita tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amefanikiwa kuokoa asilimia nne ya bajeti yake ya kwanza katika hatua alizochukua katika kubana matumizi na kudhibiti ufisadi. Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka jana alianza kwa kusisitiza kubana matumizi ya Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali, jambo alilolifanikisha kulingana na ripoti za kila mwezi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). TRA ilitangaza kukusanya Sh1.4 trilioni Desemba mwaka jana, Januari ikakusanya Sh1.08 trilioni na Sh1.04 trilioni Februari kabla haijakusanya Sh1.316 triioni mwezi Machi. Makusanyo hayo yote yalikuwa ni zaidi ya matarajio. Licha ya mapato hayo yaliyokusanywa kwa taratibu za mamlaka hiyo, Rais Magufuli amefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh1.02 trilioni ndani ya muda aliokaa madarakani. Serikali imependekeza bajeti ya Sh29.5 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha. Akisoma makadirio ya mapato na matumizi hayo kwenye kamati za Bunge, Waziri wa Fedha na Mip...