Mhasibu Tanesco jela miaka 425
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kifungo cha miaka 425, aliyekuwa Mhasibu Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lilian Chengula (42) baada ya kupatikana na hatia ya makosa 85 likiwemo la kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.3. Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi alisema mshtakiwa amepatikana na hatia ya makosa 85 kati 167 yaliyokuwa yanamkabili na katika kila kosa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela. Hata hivyo alisema, Chengula atatumikia adhabu hiyo kwa wakati mmoja ambayo itakuwa ni sawa na kifungo cha miaka mitano jela. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shahidi alisema mshtakiwa akimaliza kutumikia kifungo chake, atatakiwa kulipa zaidi ya shilingi bilioni moja. Aidha aliwaachia huru washtakiwa wenzake watatu, ambao ni mfanyabiashara Salha Salim Saad (57), Salum Saad Ally (65) na Bakary Kinyogoli (65). Alisema anawaachia huru washtakiwa hao kwa kuwa hawajatiwa hatiani katika makosa 82 yaliyokuwa yakiwakabili wote wanne. Katika kesi hiyo u...