Mchumi: TRA haiwezi Kukusanya Kodi ya Majengo
Mchumi na mtafiti wa uchumi amesema uamuzi wa Serikali kuipa Mamlaka ya Kodi (TRA) kazi ya kukusanya kodi ya majengo badala ya halmashauri za wilaya, utapunguza mapato hayo kutokana na upungufu wa rasilimali watu. Akitoa maoni yake kuhusu bajeti ya mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni juzi, mchumi huyo, Simon Mapolu alisema TRA haitamudu kukusanya mapato hayo kwa ufanisi kutokana na kuhitaji mtandao mpana wa watumishi kuweza kufanya kazi zilizokuwa zikifanywa na halmashauri za wilaya, manispaa na majiji. “Halmashauri za wilaya zina watumishi hadi ngazi ya mtaa kwa maana ya wenyeviti na watendaji wa mitaa au vijiji ambao wanatumika kufuatilia na kukusanya ushuru wa majengo, wakati TRA watumishi wao huishia ngazi ya wilaya na maeneo machache kwenye vituo maalumu,” alisema Mapolu. “Wakati Sheria ya Kodi ya Mwaka 2004 inawafanya TRA kuwasubiria walipakodi wawafuate ofisini, mamlaka za halmashauri huwafuata walipa kodi ya majengo hukohuko waliko.” K...