Rais Magufuli Awageukia Watumishi HEWA Ndani ya CCM
Rais John Magufuli juzi aliwazungumzia makada walioihama CCM wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita, alipoeleza kuwa kuondoka kwao pengine kulimsaidia kupata ushindi. Bila kutaja majina ya waliokihama chama, Magufuli alisema ni vyema wana CCM wakasahau tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo na kuganga yajayo. Rais alisema hayo kwenye mkutano na viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya zote nchini, uliofanyika juzi Ikulu jijini Dar es Salaam. Alisema kuna mengi yalitokea wakati wa uchaguzi huo na yalikidhoofisha chama na hivyo kuna haja ya kuyasahau yaliyopita na kuangalia mbele katika kukijenga chama. “Lakini inawezekana wale walioamua kwenda kule walisaidia mimi kushinda,” alisema bila ya kufafanua. Baadhi ya wana CCM waliokihama chama hicho wakati wa uchaguzi huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa kuanzia ndani ya chama hicho ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowasa aliyehamia Chadema, Frederick Sumaye, ambaye kwanza alitangaza kujiunga na upinzani...