Paul Makonda Atangaza Mikakati Itakayolifanya Jiji La Dar es Salaam Liwe la Kisasa
Siku chache baada ya kuapishwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekuja na mikakati kadhaa ikilenga kubadilisha mwonekano wa jiji hilo na kulifanya liwe la kisasa. Miongoni mwa mambo aliyoyagusia ni usafi, ofisi za Serikali kutokuwa za chama, kutenga maeneo ya biashara, sensa ya nyumba kwa nyumba, usalama wa raia na mali zao, watumishi hewa, kurudisha hadhi ya watendaji wa Serikali za Mitaa, elimu na barabara. Alitoa mikakati hiyo jana alipokuwa akizungumza na wenyeviti na watendaji wa mitaa 559 ya jiji la Dar es Salaam katika mkutano wa kujitambulisha kwao. Usafi Kuhusu usafi, Makonda alitangaza zawadi ya gari la Sh20 milioni au fedha taslimu kwa mwenyekiti ambaye mtaa wake utaongoza kwa usafi na Sh5 milioni kwa kila mjumbe wa mtaa husika. Zawadi hiyo itakayokuwa ikitolewa kila baada ya miezi mitatu, itaanza rasmi Aprili Mosi. Pia, aliahidi kutoa pikipiki 30 kwa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam ili kuwawezesha askari kuwafuatilia watu watakaotu...