Tume ya Pamoja Kufuatilia Ziara ya Rais Magufuli Nchini Rwanda
Kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyika kuanzia tarehe 29 – 30 Aprili, 2016, kimekamilika Mjini Gisenyi, Rwanda, ambapo wataalam wa sekta mbalimbali wameazimia kuharakisha maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Kikao hicho cha 14 cha ushirikiano kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa Tanzania na Rwanda wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nchini Rwanda mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu. Wakati wa ziara hiyo, wakuu hao walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano na kuibua maeneo mapya yanayolenga kuinua shughuli za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili. Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho cha wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania aliwakumbusha wajumbe wa pande zote mbili kuendesha mazungumzo na mjadala kwa kuzingatia maagizo ya viongozi hao na vilevile kuchangamkia ...