Kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyika kuanzia tarehe 29 – 30 Aprili, 2016, kimekamilika Mjini Gisenyi, Rwanda, ambapo wataalam wa sekta mbalimbali wameazimia kuharakisha maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Kikao hicho cha 14 cha ushirikiano kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa Tanzania na Rwanda wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nchini Rwanda mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Wakati wa ziara hiyo, wakuu hao walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano na kuibua maeneo mapya yanayolenga kuinua shughuli za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho cha wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania aliwakumbusha wajumbe wa pande zote mbili kuendesha mazungumzo na mjadala kwa kuzingatia maagizo ya viongozi hao na vilevile kuchangamkia fursa za ushirikiano wa shughuli za kiuchumi za wananchi wa pande zote mbili baada ya mindombinu ya kikanda kuimarika.
Kwa upande wake, Balozi Jeanine Kambanda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda na mwenyeji wa kikao hicho, alihimiza wajumbe kujiwekea malengo yanayotekelezeka na tarehe za ukomo kwenye maeneo yote watakayokubaliana ili kusukuma utekelezaji na kupata matokeo ya haraka.
Pamoja na mambo mengine, pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu kama vile miundombinu ya ushoroba wa kati (central corridor), kuharakisha ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kimataifa (standard gauge), kukuza ushirikiano katika sekta ya anga hususan baina ya mashirika ya ndege ya Rwandair na ATCL, kuimarisha ushirikiano katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, kilimo na ufugaji, utalii, elimu, mawasiliano n.k.
Mkutano huo pia umekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji (Joint Implementation Committee) kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu maeneo yote ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika Kikao hicho cha 14. Kamati hiyo itakayoongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo mbili, itakutana kila robo mwaka.
Aidha, Serikali ya Rwanda imeonesha utayari wake wa kuleta nchini Maafisa na Watumishi wa Serikali kwa lengo la kupata uzoefu na mafunzo katika vyuo vya kitaalamu nchini kama vile Chuo cha Diplomasia (CFR), Chuo cha Taifa cha Utalii na Wanyamapori (Mweka) na Chuo cha Usafirishaji (NIT).
Kwa upande wa Tanzania, Serikali imedhamiria kuwakutanisha wataalamu wa mitaala ya elimu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Rwanda kwenye upande wa kuandaa mitaala ya elimu ya tehama kwenye shule za awali, msingi na sekondari.
Mkutano ujao wa kumi na tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda utafanyika mwaka 2018, nchini Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Gisenyi, Rwanda
30 Aprili, 2016