Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hakuna mtu anayeweza kupata mafanikio kwa kuanzia juu.
Askofu Gwajima amesema hayo leo Jumatatu Desemba 25,2017 akihubiri katika ibada ya Krismasi. Amesema anayeanzia juu ipo siku atashuka chini.
Amesema kwa kawaida mafanikio ya mwanadamu yeyote duniani ni lazima yaanzie chini.
"Hata Yesu alizaliwa kwenye hori la ng'ombe, sehemu ya chini kabisa lakini ndiye aliyetukomboa na dhambi. Ogopa kilichozaliwa kwenye hori, ukiona mtu ameanzia juu jua kuna siku atashuka," amesema.
Askofu Gwajima amesema ingewezekana Yesu kuzaliwa sehemu ya heshima lakini Mungu alitaka iwe hivyo kudhihirisha utukufu wake kwamba, kilichozaliwa kwenye hori la ng'ombe ni kikuu.
Amesema chochote kinachoonekana kinyonge na kidhaifu leo, kisidharauliwe kwa sababu ipo siku kitaheshimiwa.
Akitoa mfano amesema hata yeye alianzia chini kwa kuuza mihogo na barafu.
Amewatia moyo waumini walio hatua ya awali ya maisha akiwataka kutokata tamaa kwa sababu kuna wakati wa kuinuliwa.
"Niwaambie tu msiogope, aliyeanza kwa udhaifu atamaliza kwa heshima," amesema.
Amewataka kujenga tabia ya kuwasikiliza hata wale aliowaita waropokaji kwa sababu kuna wakati Mungu anaweza kuwatumia wakawa na ujumbe wenye kujenga.