Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, amelaani kitendo cha kutishiwa kwa silaha ya moto aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Amesema kwamba, kitendo kilichofanyika dhidi ya Nape ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu na utawala bora ambacho hakiwezi kuvumiliwa.
Mgeja, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, kabla hajahamia Chadema mwaka juzi, alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma.
Pamoja na hayo, alimuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, asimame hadharani kuwaomba radhi Watanzania kwa niaba ya Serikali.
“Mbali ya kuwaomba radhi Watanzania, waziri mkuu achukue hatua mara moja ya kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo kuheshimu misingi ya demokrasia kwa kuzingatia katiba ya nchi, sheria, kanuni na taratibu,” alisema Mgeja.
Akifafanua zaidi, mwanasiasa huyo alisema tukio la Nape kutishiwa silaha ni moja ya matukio ya ukandamizaji wa haki za binadamu yanayoendelea kutokea nchini na kwamba yanatakiwa kukemewa kabla hayajaleta madhara zaidi kwa wananchi.
“Kwa kweli mimi binafsi pamoja na taasisi yangu ya Tanzania Mzalendo Foundation, tunalaani vikali kitendo kilichotendwa hadharani na mmoja wa walinzi wa raia.
“Yaani kitendo cha kumtisha raia kwa silaha ya moto kwa lengo tu la kumzuia asizungumze na wanahabari hakikubaliki, tukio hili limetushtua na kutusikitisha Watanzania.
“Matukio haya ni ishara ya wazi ya ukandamizaji wa demokrasia na ni matumizi mabaya ya madaraka ambayo yameanza kushika kasi miongoni mwa viongozi wa Serikali.
“Wananchi wengi hivi sasa hawatendewi haki, angalieni yanayotokea kwa wafugaji, ikiwamo tukio la hivi karibuni ambalo vijana wawili wa kifugaji kule Bagamoyo walipigwa risasi na kufariki.
“Wananchi wanyonge hivi sasa wanajiuliza iwapo mtu aliyekuwa waziri wa Serikali na kada maarufu ndani ya chama tawala na aliyekipigania kiweze kupata ushindi japokuwa kwa goli la mkono, leo anafanyiwa vitendo vya aina hiyo.
“Kwa kuwa sikufurahishwa na tukio hilo, namshauri Waziri Mkuu Majaliwa, asimame hadharani kwa niaba ya Serikali ya CCM, awaombe radhi Watanzania.
“Tena awahakikishie matukio ya aina hiyo hayajirudii tena kwa sababu yeye na viongozi wengine, waliapa kuilinda Katiba na siyo kuivunja,” alisema Mgeja.