Bandari Ya Dar es Salaam Kuunganisha Singapore Na Afrika Mashariki
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dk. Koh Poh Koon, amesema wamepanga kutumia bandari ya Dar es Salaam kuwa kiunganishi cha biashara kati ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika Mashariki. Dk. Koon ameyasema hayo jana(Jumatano, Aprili 27, 2016), wakati alipomtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma, na kwamba Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za Tanzania. Dk. Koon ambaye ameambatana na wafanyabiashara wakubwa wapatao 40, amemweleza Waziri Mkuu kwamba kampuni ya Hyflux ya Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi (Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati (light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo 37,000. “Jiwe la msingi la mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili...