SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 5 Mei 2016

T media news

Rais Magufuli Aokoa Asilimia 4 ya Bajeti


Ndani ya miezi sita tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amefanikiwa kuokoa asilimia nne ya bajeti yake ya kwanza katika hatua alizochukua katika kubana matumizi na kudhibiti ufisadi.

Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba  5, mwaka jana alianza kwa kusisitiza kubana matumizi ya Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali, jambo alilolifanikisha kulingana na ripoti za kila mwezi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

TRA ilitangaza kukusanya Sh1.4 trilioni Desemba mwaka jana, Januari ikakusanya Sh1.08 trilioni na Sh1.04 trilioni Februari kabla haijakusanya Sh1.316 triioni mwezi Machi.

Makusanyo hayo yote yalikuwa ni zaidi ya matarajio. Licha ya mapato hayo yaliyokusanywa kwa taratibu za mamlaka hiyo, Rais Magufuli amefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh1.02 trilioni ndani ya muda aliokaa madarakani.

Serikali imependekeza bajeti ya Sh29.5 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha. Akisoma makadirio ya mapato na matumizi hayo kwenye kamati za Bunge, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Sh17.7 trilioni zitakuwa ni za matumizi ya kawaida na Sh11.8 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

Kiasi kilichookolewa na Rais Magufuli  ni takribani nusu ya mapato yatakayotokana na vyanzo visivyo vya kodi na pia zaidi ya mara mbili ya mapato yatakayokusanywa na halmashauri zote nchini kwa kipindi hicho.

Ni fedha nyingi zikilinganishwa na zile zilotolewa na Shirika la Msaada la Marekani (MCC) awamu ya kwanza kutekeleza usambazaji wa umeme vijijini. Ndani ya siku 30 za kwanza; baada ya kufanya safari ya kushtukiza hazina na kutembelea bandarini mara kadhaa aliokoa takribani Sh1 trilioni.

Makontena zaidi ya 2,500 yaliyobainika kuondoshwa bila kulipiwa ushuru na tozo nyinginezo yaliipa Serikali Sh637.2 bilioni. Fedha hizo zilitokana na malipo ya lazima pamoja na faini kwa wakwepaji.

Bado Novemba mwaka jana wakati anazindua Bunge, Rais alikataa kufanya sherehe zilizoandaliwa na wabunge na akaagiza Sh225 milioni zielekezwe kwenye maeneo yenye uhitaji. Maamuzi hayo yalizipeleka fedha hizo kununua vitanda 300, magodoro 300, mablanketi 1,675 na viti vya magurudumu 30 ambavyo vilikabidhiwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Kwenye mkutano huo, Rais aliliambia Bunge kuwa hatua yake ya kuzuia safari za nje kwa watumishi wa umma imeokoa Sh356.3 bilioni ambazo zinaweza kujenga kilometa 400 za barabara ya lami.

Desemba 9, mwaka jana, Dk Magufuli aliahirisha sherehe za uhuru na akaagiza Sh4 bilioni zilizotengwa zitumike kupanua barabara kutoka Morocco mpaka Mwenge, jijini hapa. Utekelezaji wa agizo hilo unaendelea.

Muda mfupi baada ya kuteua mawaziri na manaibu wao, alifuta semina elekezi kwa viongozi hao. Hapa aliokoa Sh2 bilioni ambazo zilipangiwa matumizi mengine.

Mapema Aprili alifuta sherehe za Maadhimisho ya Muungano na kuelekeza Sh2 bilioni zilizotengwa kwa ajili hiyo zitumike kupanua barabara ya Uwanja wa Ndege-Mwanza.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni kuunga mkono juhudi za kubana matumizi, Bunge liliokoa Sh6 bilioni ambazo ilizikabidhi kwa Rais ili zinunue madawati kwa shule zenye upungufu nchini.