MICHEZO:mwamuzi wa uwanjani ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya maamuzi yote yanayofanyika wakati wa mechi.
"Katika soka, Sheria za Mchezo ziko wazi kabisa: mwamuzi wa uwanjani ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya maamuzi yote yanayofanyika wakati wa mechi. Mara tu mchezo unapoendelea na kukamilika, matokeo yaliyopatikana uwanjani yanapaswa kubaki kama yalivyo.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Afrika CAF, waamuzi na maofisa wa mechi wana mamlaka kamili wakati wa mchezo.
Kanuni za CAF zinaendana na Sheria za Mchezo za FIFA, ambazo zinaeleza kwamba:
Mwamuzi ana mamlaka kamili ya kusimamia utekelezaji wa Sheria za Mchezo katika mechi aliyopangiwa, na maamuzi yake kuhusu matukio yanayohusiana na mchezo ni ya mwisho.
Sheria ya 5 ya Sheria za Mchezo, inayotumika katika mashindano yote ya mashirikisho ikiwemo CAF.
Katika kesi ya fainali ya AFCON kati ya Senegal na Morocco, mwamuzi aliruhusu mchezo kuendelea baada ya kitendo cha Senegal kutoka uwanjani kwa muda, na mechi ikakamilika hadi mwisho, ikiwemo muda wa nyongeza, huku matokeo yakipatikana uwanjani.
Zaidi ya hayo, baada ya mechi, ripoti ya mwamuzi ilibainisha kuwa kulikuwa na kusimama kwa mchezo kwa muda, na siyo kupoteza mechi kwa kutofika au kugomea kabisa kucheza. Pia alipendekeza adhabu stahiki kwa makosa yaliyotokea wakati wa mchezo.
Kwa sababu hiyo, uamuzi uliofuata wa kamati ya CAF baada ya mechi kumalizika haupaswi kufuta au kupuuza mamlaka yaliyotumiwa na mwamuzi wakati wa mchezo kwa mujibu wa Sheria ya 5 ya Sheria za Mchezo.
Soka linapaswa kuamuliwa uwanjani, siyo kubadilishwa matokeo baada ya filimbi ya mwisho.
Hakuna msingi wa kimichezo wa kufuta matokeo ya mechi iliyokamilika kwa mujibu wa mamlaka ya mwamuzi na Sheria za Mchezo. Vinginevyo, soka litaingia katika njia hatari ambapo maamuzi ya waamuzi wa uwanjani kuhusu penalti, kuotea na kadi nyekundu yataanza kubatilishwa na viongozi wa kamati baada ya mechi kumalizika.
Je, hali hiyo itaishia wapi?
Uamuzi huu umeendelea kulichafua soka la Afrika na kudhoofisha imani ya watu katika usawa, uthabiti na uadilifu wa mchezo huu barani Afrika.
Ninaiomba Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo CAS pamoja na mamlaka nyingine husika kuchukua hatua za haraka na za wazi ili kuhakikisha dhuluma hii haidumu.
Pia nataka kutumia nafasi hii kuweka wazi kuwa taarifa zinazosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii zikidai kwamba ninaunga mkono uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya CAF dhidi ya Senegal ni za uongo kabisa.
Wote wanaosambaza picha yangu na kuihusisha na kauli hizo za uongo wanaombwa kuacha mara moja."
Ameandika; George Manneh Weah, Sr., Mshindi wa Ballon d’Or 1995 na Mchezaji Bora wa Afrika mara tatu 1989, 1994, 1995
