RAIS WA RWANDA AIDHINISHA KUREJESHWA KWA ADHANA YA ALFAJR

 


Rais wa  Rwanda Paul Kagame ameridhia kurejeshwa kwa adhana ya alfajiri kupitia vipaza sauti kwa Waislamu nchini humo, baada ya awali kusimamishwa kutokana na utekelezaji wa kanuni za kudhibiti kelele mijini.


Uamuzi huo unafuatia marufuku iliyotolewa mwezi Aprili mwaka 2022 na Wizara inayosimamia Serikali za Mitaa nchini Rwanda, iliyozuia matumizi ya vipaza sauti kwa adhana ya alfajiri, ikielezwa kuwa ni hatua ya kudhibiti uchafuzi wa kelele hasa katika mji wa Kigali na maeneo mengine ya mijini.


Adhana ya alfajiri ina umuhimu mkubwa katika Uislamu, ikiwa ni mwito wa kwanza kati ya swala tano za kila siku, unaotolewa kabla ya mapambazuko ya jua.


Hatua ya kurejesha adhana imekuja baada ya hoja hiyo kuwasilishwa na mmoja wa wananchi wakati wa mkutano uliojumuisha viongozi wa serikali, wawakilishi wa Waislamu pamoja na viongozi wa dini mbalimbali, uliolenga kujadili masuala ya kijamii na maendeleo ya taifa.