NAMNA YA GHUSL (KUOGA) JANABA

 


Kuoga Ghusl (Janaba) ni kuoga kwa ajili ya kujitwaharisha baada ya janaba ili mtu aweze kuswali na kufanya ibada nyingine.


Hatua za Kuoga Ghusl


1. Kuweka nia

Unanuia moyoni kuoga ili kujitwaharisha na janaba kwa ajili ya Allah.


2. Kusema Bismillah

Ni vizuri kuanza kwa kusema: Bismillah.


3. Kuosha mikono

Osha mikono yako mara tatu.


4. Kuosha sehemu za siri

Osha sehemu za siri na uondoe uchafu wowote uliopo.


5. Kutawadha udhu kama wa swala

Tawadha kama unavyotawadha kwa ajili ya swala (unaweza kuacha kuosha miguu mpaka mwisho).


6. Kumimina maji kichwani

Mimina maji kichwani mara tatu na hakikisha maji yanafika kwenye ngozi ya kichwa na mizizi ya nywele.


7. Kuosha mwili wote

Osha mwili wote ukianza upande wa kulia kisha kushoto, na hakikisha maji yanafika sehemu zote za mwili.


8. Kuosha miguu

Ikiwa hukuosha miguu wakati wa udhu, basi ioshe mwisho wa kuoga.


📃Dalili kutoka Sunnah


Aisha (RA) amesema:


“Mtume ï·º alipokuwa akioga janaba, alianza kwa kuosha mikono yake, kisha akatawadha kama udhu wa swala, kisha akapitisha vidole vyake kwenye nywele zake na kumimina maji kichwani mara tatu, kisha akaosha mwili wake wote.”

(Bukhari na Muslim)


🌿Kuoga Ghusl kwa mwanamke


Namna ya kuoga Ghusl kwa mwanamke ni sawa na mwanaume.


Lakini ikiwa mwanamke ana nywele zilizosukwa, si lazima kuzifungua. Inatosha kujimina maji kichwani na kuhakikisha maji yanafika kwenye ngozi ya kichwa.


Ikiwa nywele zimesukwa sana na zimekaza, ni bora kuzifungua ili kuhakikisha maji yanafika vizuri kwenye ngozi ya kichwa.


📃Dalili ya Sunnah


Ummu Salamah (RA) amesema:


Mwanamke alimwambia Mtume ï·º:

“Ewe Mtume wa Allah, mimi ni mwanamke mwenye nywele nyingi zilizosukwa, je inanipasa nizifungue ili nioge janaba?”


Mtume ï·º akasema:

“Hapana, inatosha kwako kumimina viganja vitatu vya maji kichwani mwako, kisha ujimwagie maji mwili wako wote, na hivyo utakuwa umetwaharika.”(Ahmad, Muslim na Tirmidhiy – Hadith Hasan Sahih).


🌿Kumbuka ;

Chembe za maji zinazorudi kwenye chombo haziharibu maji wala josho.


Imepokewa kutoka kwa Aisha (RA) amesema:

“Nilikuwa nikioga mimi na Mtume wa Allah ï·º katika chombo kimoja, mikono yetu ikipishana ndani yake, na nilikuwa nikisema: niachie… niachie.” Na walikuwa wakifanya hivyo hali ya kuwa wote wana janaba. (Muslim)


➡️Mambo Muhimu ya Kuzingatia


🌿 Hakikisha maji yanafika sehemu zote za mwili.

🌿 Hakikisha hakuna sehemu inayobaki bila kufikiwa na maji.

🌿 Ghusl inakufanya uwe safi kwa ajili ya ibada kama Swala na kusoma Qur’an nk.