SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 4 Machi 2016

T media news

UMUHIMU WA MTI WA MPERA NA MATUNDA YAKE KIAFYA


MTI wa mpera ni miongoni mwa miti ya matunda inayofahamika na wengi hapa nchini. Mti huu hutoa matunda yanayofahamika kama mapera. Asili ya mti huu ni Amerika ya Kati na Kusini licha ya kuwa siku hizi unapatikana sehemu mbalimbali nchini na duniani kote.

Mmea huo kama ilivyo mimea mingine ya matunda, hustawi zaidi katika hali ya hewa ya kitropiki. Hapa nchini Tanzania mti huu unasadikika uliletwa na wakoloni waliotoka mashariki ya mbali waliokuja Afrika kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo suala la kueneza dini ya Kiislamu na Kikristo.

Mapera ni miongoni mwa matunda yenye kiwango kizuri cha vitamin C pamoja na vitamin A na inaelezwa kuwa kiwango cha vitamin C kinachopatikana ndani ya pera ni mara nne ya kiwango cha vitamin hiyo kinachopatikana kwenye chungwa.

Pia mapera yamesheheni virutubisho mbalimbali ikiwa ni pamoja na vitamin B2, E na K pamoja na madini ya chuma, ‘copper’, ‘potassium’ na ‘manganese.’

Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kuchapishwa na Jarida la Journal of Human Hypertension mwaka 1993 ulieleza kuwa tunda aina ya pera hupunguza kiwango cha msukumo mkubwa wa damu ndani ya mwili yaani 'High Blood Pressure' hii ni kwa sababu ya madini ya potassium na vitamin C ambayo husaidia kuweka sawa msukumo wa damu ndani ya mwili.

Faida haziishii kwenye tunda pekee, bali hata majani ya mti wake yanapoandaliwa vizuri huweza kuwa tiba ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na malaria. Majani ya mpera yanapoandaliwa kama chai, yaani yakichemshwa husaidia kuondosha sumu ndani ya mwili 'cholesterol' jambo ambalo husaidia kulinda afya ya moyo wako pia.

Majani hayo hayo ya mpera pia huwasaidia wale wenye matatizo ya kuharisha, ili kukabiliana na tatizo hilo mgonjwa wa kuhara huweza kuandaliwa maji yatokanayo na majani ya mpera ambayo yamechemshwa na kunywa kikombe kimoja asubuhi na jioni.

Vilevile majani ya mpera husaidia kutibu tatizo la vidonda vya tumbo, huku likiwa na virutubisho vingi ambavyo husaidia kuimarisha fizi na kuongeza vitamin B na A mwilini.

Majani ya mpera yenye uzito wa kilo moja yanapopondwa na kisha mgonjwa akanywa lita moja ndani ya siku nzima husaidia kukinga seli za mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Majani mateke ya mti huo yanapofungwa shingoni kwa mwenye tezi huweza kuponyesha tatizo hilo pia na mwenye jipu akifunga sehemu husika hulifanya jipu kuiva kwa haraka.

Pamoja na majani hayo kuwa msaada wa kutibu maradhi mbalimbali , halikadhalika juisi ya mapera nayo husaidia sana kutibu mgolo au bawasiri, figo na hata kuondoa mafuta katika moyo.

Kimsingi mti wa mpera karibu kila sehemu yake ni tiba kwani hata mizizi yake inapochemshwa na kutumia kwa kunywa huenda kuwasaidia wanawake wenye matatizo ya hedhi au wenye matatizo ya kutokwa na maji yenye harufu mbaya sehemu zao za siri.

Sanjari na hayo, watoto wadogo wenye matatizo ya kutopata choo zaidi ya siku mbili, wakinyweshwa maji ya majani hayo baada ya kuchemshwa huwasaidia kuondokana na shida hiyo, lakini ni vyema kuwasiliana na wataalam wa tiba asili kabla ya kuamua kutumia majani hayo kama tiba kwa mtoto.