Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania imewahakikishia Watanzania kuwa serikali ya nchi hiyo ina uhakika wa asilimia 98 za kupata mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuelekea bandari ya Tanga, mradi ambao unapiganiwa pia na nchi jirani ya Kenya.
Kufuatia hali hiyo, wizara hiyo imefanya mkutano na wafanyabiashara wa sekta ya mafuta, na kuwaeleza fursa zilizopo kwenye mradi huo, jambo ambalo limewafanya wafanyabiashara hao kuazimia kwenda nchini Uganda kwa lengo la kukutana na Serikali ya Kampala, ili kupata maelezo ya kina ya faida itakazozipata nchi hiyo kwa kuleta mradi huo nchini mwao. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, alielezea kuwepo mvutano mkubwa wa wapi mradi huo utajengwa kutokana na serikali ya Kenya kutaka mradi huo ujengwe nchini kwake. Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania, hadi kufikia juzi mazungumzo yalikuwa yangali yakiendelea kati ya Uganda na Kenya. Alisema kuwa, pamoja na hayo, Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata mradi huo kutokana na vivutio vilivyopo, ikiwa ni pamoja na gharama ndogo za ujenzi wa bomba hilo ikilinganishwa na ujenzi huo kwenda Kenya. Aliongeza kuwa, ni kutokana na kuwa na uhakika huo, ndio maana wizara yake ikaamua kufanya mkutano na wawekezaji wa sekta ya mafuta nchini Tanzania ili kuwataka waone fursa zilizopo kwenye mradi huo na zabuni ambazo wanaweza kuomba zikiwemo pia ajira zitakazopatikana katika mradi wenyewe na aina ya kodi itakayolipwa wakati wa mradi.