Rais wa zamani wa Cuba Fidel Castro amesema nchi yake inaweza kujitegemea na hivyo haihitajii misaada yoyote kutoka Marekani.
Katika makala yake ya awali tokea Rais Barack Obama aitembelee nchi hiyo Machi 20 kwa muda wa siku tatu, Castro amemtaka, ‘Ndugu Obama’ aache kutafakari na kuleta nadharia kuhusu siasa za Cuba.
Aidha amesema Cuba haiwezi kusalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani na kuongeza kuwa nchi yake ina watu wenye kujitolea na ambao wamefikia ustawi wa kielimu, kisayansi na kiutamaduni chini ya mapinduzi yaliyoiletea nchi hiyo heshima.
“Tunaweza kujizalishia chakula na utajiri kwa kutegemea kazi na uwezo wa kifikra wa watu wetu. Hatuhitajii misaada ya Markani,” alisema kiongozi wa Mapinduzi ya mwaka 1959 ya Cuba.
Castro aidha amekosoa matamshi ya Obama kuhusu demokrasia nchini humo. Amesema Obama hakutaja kuwa ubaguzi wa rangi Cuba uliondolewa kupitia mapinduzi na kwamba malipo ya uzeeni na mshahara kwa kila raia wa Cuba ni mambo yaliyopitishwa wakati Obama akiwa na umri wa miaka 10.
Castro aidha amemkumbusha Obama kuhusu namna Marekani ilivyoshirikiana na utawala haramu wa Israel kuupa silaha za nyuklia utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Katika makala hiyo yenye maneno 1,500 Castro amesema Cuba ilizisaidia nchi za Afrika kama vile Angola, Msumbiji na, Guinea Bissau kujinyakulia uhuru.
Wiki iliyopita Obama alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea Cuba katika kipindi cha miaka 90. Rais huyo wa Marekani amekuwa akijaribu kurejesha uhusiano wa kawaida wa nchi hizo mbili jirani. Cuba inasema kabla ya uhusiano kuwa wa kawaida Marekani inapaswa kusitisha mzingiro wake dhidi ya nchi hiyo na kuirejejshea eneo la Guantanamo Bay.