Makandarasi wanaojenga barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 na Kibondo-Nyakanazi Km 50 wametakiwa kukamilisha ujenzi huo mwezi Mei mwakani badala ya Novemba ili kuharakisha mkakati wa Serikali wa kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami.
Waziri
hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo uliyogawanywa sehemu mbili, Kidahwe-Kasulu inayojengwa na China Railway 50 Group na Kibondo-Nyakanazi inayojengwa na Nyanza Road Works.
Prof. Mbarawa amewataka makandarasi hao kuongeza kasi ya ujenzi, vifaa na wafanyakazi wenye sifa ili barabara hizo zikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.
“Tutahakikisha ifikapo Juni mwaka huu tutakuwa tumelipa madeni yote mnayoidai Serikali hivyo fanyeni kazi kwa uhakika kwa kuwa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano tayari tumeshawalipa makandarasi zaidi ya shilingi bilioni 725”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza kwamba nia ya Serikali ni kuifungua mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa kwa barabara za lami ili kufungua ukanda wa magharibi mwa nchi kibiashara kutokana na ukanda huo kuwa sehemu muhimu ya nchi katika uzalishaji na kiungo kikuu kwa nchi za Congo DRC, Burundi na Rwanda.