Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi wa kesi za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia, zinazowakabili askari wa kofia ya buluu wa umoja huo ambao wanahudumu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ripoti iliyotolewa na kikosi cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, (MINUSCA) imesema kuwa, ni suala muhimu kufanyika uchunguzi huo kwa lengo la kubaini au kuthibitisha tuhuma hizo dhidi ya askari wake. Uchunguzi huo unasimamiwa na Diane Corner, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ripoti ya MINUSCA imeongeza kuwa, natija ya uchunguzi huo itawasilishwa kwa nchi wanakotoka askari hao ambapo nchi hizo nazo zitachukua hatua madhubuti kuwahusu askari wake. Hatua hiyo imekuja baada ya kuripotiwa kwa kesi kadhaa za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo na wanawake zinazowahusu askari wa kusimamia usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambazo zimekuwa zikiripotiwa tangu mwaka 2014 na 2015 katika eneo la Kémo.