SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 30 Machi 2016

T media news

Saudia muhusika mkuu katika kushuka kwa bei ya mafuta duniani


Saudia muhusika mkuu katika kushuka kwa bei ya mafuta duniani
Kuendelea kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kumeendelea kuathiri uchumi wa nchi zinazozalisha nishati hiyo muhimu. Inakadiriwa kuwa, bei ya mafuta katika mwaka huu wa 2016 itaendelea kusalia karibu Dola 40 au chini kwa pipa, na hivyo kupigilia msumari wa matatizo kwenye msingi wa uchumi wa nchi hizo.
Hii ni kusema kuwa, tangu mwaka 2014 bei ya mafuta imeendelea kushuka kwa karibu asilimia 75 kutoka Dola 140 na kufikia karibu Dola 30 kwa pipa. Kufuatia hali hiyo, Benki ya Société Générale, ambayo ni moja ya benki kubwa za Ulaya imetabiri kuwa, kutoongezeka kiwango cha matumizi ya mafuita nchini Marekani na katika masoko yanayoinukia kiuchumi, ni jambo ambalo litasababisha uzalishaji wa ziada wa mafuta kuendelea kushuhudiwa duniani. Uzalisha ulio zaidi ya kiwango kilichoainishwa na Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) unaofanywa na Saudi Arabia, ndio umeharibu bei ya mafuta duniani. Miezi michache iliyopita, Saudia na Russia ambazo zinashika nafasi ya pili na ya tatu katika uzalishaji mafuta duniani baada ya Marekani, zilikubaliana kutozalisha mafuta zaidi ya kiwango na badala yake zipunguze uzalishaji huo kwa kiwango kilicho chini ya kiwango cha uzalishaji wa mwezi Januari mwaka jana, katika hali ambayo hadi sasa nchi hizo hazijaifanyia kazi ahadi hiyo. Kwa mujibu wa gazeti la Washington Times, makubaliano hayo ya Saudia na Russia hayakuwa na natija yoyote katika kuinua bei ya nishati hiyo muhimu katika soko la dunia. Baadhi ya weledi wa mamabo wanaamini kwamba, licha ya kuongezeka mahitaji ya mafuta kwa Uchina ambayo ni moja ya wanunuzi wakubwa wa mafuta duniani, bado uchumi wa nchi hiyo umeendelea kudorora, suala ambalo linatia wasi wasi mkubwa. Sambamba na kuendelea kushuka kwa bei ya mafuta, wazalishaji wa nishati hiyo kwa njia ya Shale, ambao ni mfumo wa uzalishaji mafuta katika matabaka ya changarawe na mawe, na ambao ni uzalishaji wa gharama kubwa, wamekumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na hata kulazimika kusimamisha shughuli hiyo. Mwezi uliopita taasisi ya uchunguzi wa uchumi ya kimataifa ya Peterson Institute for International Economics ilitangaza kuwa hatari ya mchezo huo wa kamari wa pata-potea unaochezwa hivi sasa na Saudi Arabia ni kubwa zaidi kuliko inavyodhania. Taasisi hiyo iliyo na makao yake nchini Marekani imeelezea makosa ya kisiasa yalitofanywa na Saudia kwa kuandika kuwa, miamala iliyochukuliwa na watawala wa Aal Saudi kufuatia kutiwa saini makubaliano ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilikuwa ya kiwendawazimu. Saudia ilichukua hatua hiyo kutokana na wasi wasi wake kwamba, baada ya makubaliano hayo Iran ingeweza kuimarisha nafasi yake katika soko la mafuta duniani. Hii ni kusema kuwa, tangu mwaka 2012 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kufuatia kuwekewa vikwazo vya kidhalimu, iliendelea kusalia nyuma katika soko hilo. Hata hivyo hali ya mambo imebadilika na sasa mlango huo iliokuwa umefungiwa nchi hii umefunguliwa. Viongozi wa Riyadh walitarajia kuona mporomoko wa bei ya mafuta katika soko la mafuta duniani, ukitoa pigo kubwa kwa uchumi wa taifa hili. Ukweli ni kwamba, hatari kubwa inayotokana na mporomoko wa bei ya mafuta duniani, imezikumba nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, athari za kisiasa zilizosababishwa na bei mbaya ya mafuta duniani, imeharibu sana uchumi wa nchi za Saudia na Kuwait. Hasa kwa kuzingatia kuwa, nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi zimewekeza kiasi kikubwa cha mabilioni ya dola kwenye sekta ya ulinzi na ununuzi wa silaha za kisasa. Nchi hizo ambazo ziko kwenye kilele cha mgogoro wa kiuchumi, bila shaka zitakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumi endapo zitaendelea kufuata kibubusa siasa za kupenda kujitanua za Saudi Arabia.