DAR ES SALAAM
KAMPUNI inayojihusisha na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Mwanza na Tabora ya Chico CCC ya China, imepewa muda wa miezi miwili ya kuhakikisha imekamilisha miradi yake ya umeme.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokutana na kampuni hiyo ofisini kwake Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi yake ya umeme vijijini. Kampuni hiyo inatekeleza miradi ya umeme inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mara baada ya kupokea taarifa hiyo na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kampuni hiyo, Profesa Muhongo aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inakamilisha miradi yake ifikapo mapema Mei mwaka huu.
Alisisitiza kuwa wananchi wanahitaji umeme wa uhakika, ambao ni nguzo ya ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia viwanda, hivyo serikali haitamwonea haya mwekezaji yeyote asiyetekeleza mradi wa umeme aliopewa kwa kasi inayoridhishwa.