SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 30 Machi 2016

T media news

UGONJWA WA MDUDU WA KIDOLE!







Ugojwa wa mdudu wa kidole ni kitu gani?
Katika mila na desturi zetu, kuna ugonjwa ambao umezoeleka kuitwa mdudu wa kidole. Katika mila na desturi hizi, inaaminika kuwa kuna mdudu ameingia kwenye kidole, mara nyingi chini ya ukucha, ambaye anasababisha kidole husika kikumbwe na maumivu makali sana. Hata hivyo katika taaluma ya tiba hali haiko hivyo. Kilichoko ni kwamba ni kweli kidole kinakumbwa na maambukizi, lakini maambukizi yenyewe siyo ya mdudu unayeweza kumwona kwa macho, na pia siyo maambukizi ya aina moja.
Kitaalamu aina za maambukizi kwenye kidole yanayopelekea kuzaliwa kwa maumivu makali yako aina tano tofauti. Mara nyingi maambukizi husika hutokana na bakteria, isipokuwa aina moja tu. Aina hii ni ile inayojulikana kama Herpetic whitlow, ambayo husababishwa na kirusi. Kwa kawaida ili maambukizi yatokee ni lazima kwanza kuwe na jeraha. Jeraha linaweza kuwa ni la kujikata, kung’atwa na mdudu, au kujitoboa.

Maambukizi katika kidole huzaa dalili zinazotofautiana kwa kiasi fulani kwa kutegemea na eneo lililoambukizwa. Hii ina maana kuwa kutambua maambukizi mahsusi yanayohusika katika kesi fulani ni kitu kinachowezekana. Tofauti za maambukizi ya kidole ni hizi zifuatazo:
Paronychia:
Katika aina hii ya maambukizi, eneo la kidole linalopakana na kucha linabadilika rangi na kuwa jekundu na huku likiwa limevimba. Kunakuwa na mkusanyiko wa usaha unaoonekana chini ya ngozi na kucha. Eneo lilioathirika linakula laini na unapoligusa unapata maumivu makali. Iwapo utatoboa eneo husika usaha utakaotoka utakuwa na rangi mchanganyiko wa weupe wa ukungu na njano.
Felon:
Katika aina hii ya maambukizi, ncha ya kidole inakuwa imevimba na yenye kutoa maumivu. Kwa kawaida uvimbe huanza taratibu na kuendelea katika kipindi cha siku kadhaa, na mara nyingi upo upande wa chini wa ncha ya kidole, upande ule wenye nyama laini. Eneo lililoathrika mara nyingi linakuwa na maumivu yanayopwita, na ukiligusa pia hutoa maumivu makali. Eneo husika linakuwa na rangi nyekundu na chini ya ngozi unaweza kuonekana usaha. Eneo husika linaweza kuwa na kipande ambacho kimelainika kana kwamba kuna kimiminika ndani. Kadri uvimbe unavyoongezeka eneo husika linaweza kubadilika na kuonekana kama gumu pale linapoguswa.
Herpetic whitlow:
Katika aina hii ya maambukizi, eneo la ncha ya kidole linakuwa laini na lenye rangi nyekundu. Maumivu kama ya kuungua hivi yanaweza yakahisiwa pia katika eneo hilo. Kunaweza pia kuwa na kiasi fulani cha uvimbe lakini siyo kwa kiwango kinachofikia maambukizi ya felon. Kunaweza pia kuwa na jeraha la wazi au majeraha kadhaa ya wazi katika eneo husika. Kwa kawaida majeraha haya huwa yanajilundika katika eneo moja na hutokea baada kutokea kwa mkusanyiko wa vilengelenge kadhaa. Majimaji yanayotoka katika majeraha haya mara nyingi hayana rangi japokuwa kuna wakati yanakuwa na rangi kama ya ukungu. Mtu alipata maambukizi haya anaweza pia kujisikia homa na pia akavimba mitoki iliyoko jirani na eneo lenye maambukizi.
Cellulitis:
Katika aina hii ya maambukizi, ngozi katika eneo husika huwa nyekundu na yenye joto. Eneo husika linaweza pia kukabiliwa na uvimbe mdogo na pia kuwa laini. Kwa kawaida haya maambukizi ni ya juu juu na hayahusishi tishu za ndani. Kwa kawaida kidole husika au mkono wenye kidole hicho unaposogea hakuna maumivu yoyote makali yanayomkumba mhusika.
Infectious flexor tenosynovitis:
Kwa kawaida kuna dalili nne kubwa katika aina hii ya maambukizi.
Kwanza:
Ni kulainika kwa upande wa chini wa kidole (tumbo la kidole) kunakoambatana na maumivu ya mishipa katika eneo hilo.
Mbili:
Ni uvimbe uliosambaa katika kidole chote.
Tatu:
Ni maumivu kila mhusika anapojaribu kukinyoosha kidole hicho.
Nne:
Kidole kinakuwa kimekaa katika mkao wa kujikunja kidogo.
Deep space infections:
Katika aina hii ya maambukizi huitwa pia collar button abscess. Haya ni maambukizi yanayojitokeza katika eneo linalotenganisha vidole viwili. Eneo hili ilakuwa na uvimbe na maumivu. Aidha eneo husika linaweza kuwa na rangi nyekundu na lenye joto. Kadri jipu lililopo linavyozidi kuwa kubwa ndivyo vidole vitakavyozidi kuachana. Eneo la kati linaweza kuwa na ncha laini inayoweza kuwa ni dalili ya kuwepo kwa usaha chini ya ngozi.
MATIBABU
Kihospitali, maambukizi takriban yote ya kidole hutibiwa kwa vijaua vijasumu (antibiotics) na uangalizi sahihi wa jeraha katika eneo lililoathirika. Uangalizi sahihi wa jeraha utatofautiana kulingana na aina ya maambukizi yanayohusika. Uangalizi huu unaweza kuwa ule mwepesi kabisa kama kutoboa kidogo na kukamua hadi usaha wote umalizike, hadi ule ambao unahusisha upasuaji wa kina wenye nia ya kuondoa sehemu kubwa ya tishu zilizoambukizwa kadri inavyowezekana.
Baadhi ya haya maambukizi hutibiwa na mgonjwa kuruhusiwa kurudi nyumbani, lakini mengine yanaweza kuhitaji mgonjwa kulazwa na kupewa vijaua vijasumu kwa njia ya dripu.
Kwa upande wa tiba mbadala au tiba asili, matibabu mara nyingi huhusisha kusafisha eneo lililoathirika na kulifunga dawa. Ziko dawa nyingi zinazotumika kwa kazi hiyo lakini moja ambayo ni mujarabu sana, na ambayo haihitaji kumwona tabibu ni kitunguu.
Baada ya eneo husika kusafishwa vizuri kidole chote huzungushiwa kitunguu kilichopondwa na kushikanishwa hapo kwa bandeji. Dawa hii ni mujarabu sana kiasi kwamba mgonjwa anaweza kupoa kabisa ndani ya saa 24 tangu aanze kuumwa. Kama ukipata tatizo la maambukizi ya kidole unaweza ukaijaribu tiba hii, kabla ya kuamua kutafuta tiba za kihospitali iwapo itabidi.