Rais Barack Obama wa Marekani ametahadharisha kuhusiana na matokeo mabaya ya kuenea utumiaji wa madawa ya kulevya katika nchi hiyo.
Obama amesema hayo katika mkutano wa kukabiliana na matumizi ya madawa ya kulevya mjini Washington na kubainisha kwamba, idadi ya watu wanaopoteza maisha yao kutokana na utumiaji wa madawa ya kulevya ni zaidi ya wale wanaofariki dunia kutokana na ajali za barabarani. Rais Obama ameongeza kuwa, uraibu wa madawa ya kulevya umekuwa na taathira mbaya kwa matabaka yote ya jamii kuanzia familia, watoto, wanasiasa mpaka kwa wananchi wa kawaida. Rais wa Marekani aidha amesema kuwa, sera za Washington za kukabiliana na magendo ya madawa ya kulevya hadi sasa hazijazaa matunda. Marekani ndio soko kubwa zaidi duniani la magendo ya madawa ya kulevya. Uchunguzi unaonesha kuwa, kati ya kila raia elfu moja wa Marekani, 61 kati yao hutumia afyuni na mfano wa hayo na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza duniani katika uwanja huo. Katika miongo ya hivi karibuni watu laki tatu nchini Marekani wameongezeka katika idadi ya watumiaji wa madawa ya kulevya aina ya heroini. Fauka ya hayo, Marekani na Uhispania zinaongoza duniani kwa kuwa na watu wengi wanaotumia madawa ya kulevya aina ya kokeini. Takwimu hizo zinaongezeka katika hali ambayo Marekani ina taasisi kubwa zaidi duniani ya kupambana na madawa ya kulevya. Idara ya Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini Marekani iliasisiwa mwaka 1973 na kwa sasa ina wafanyakazi zaidi ya elfu kumi na imekuwa ikipewa bajeti ya dola bilioni 2 kila mwaka. Pamoja na hayo, idara hiyo ikishirikiana na taasisi nyingine kama vyombo vya mahakama na polisi ya FBI haijaweza kuzuia mwenendo wa ongezeko la utumiaji wa madawa ya kulevya nchini humo. Katika barabara na mitaa mingi ya Marekani hususan katika maeneo ya watu masikini, madawa ya kulevya yanapatikana kwa urahisi na yanauzwa na kununuliwa kwa bei nafuu kabisa. Aidha katika baadhi ya majimbo ya Marekani utumiaji wa madawa ya kulevya aina ya bangi hata katika masuala yasiyo ya kitiba ni jambo linaloruhusiwa baada ya kupasishwa kupitia kura ya maoni. Inaelezwa kuwa, takribani asilimia 70 ya wananchi wa Marekani kwa akali wametumia bangi japo mara moja katika kipindi cha maisha yao. Ushahidi mwingi uliopo unaonesha kuwa, baadhi ya watumiaji wa madawa mengine ya kulevya kama kokeini au afyuni awali waliwahi kuvuta bangi. Hii ni katika hali ambayo, kuna magenge mengi ya kimafia yenye nguvu nchini Marekani ambayo yanahodhi uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa madawa ya kulevya sio katika nchi hiyo tu bali katika maeneo mbalimbali duniani. Magenge hayo yana maelfu ya watu wenye silaha ambao nguvu zao za kijeshi zinalingana na majeshi ya baadhi ya nchi. Kila mwaka maelfu ya watu huuawa ndani na nje ya Marekani kutokana na vitendo vya utumiaji mabavu vinavyofanywa na mamafia wa madawa ya kulevya. Magenge ya madawa ya kulevya yakitumia vitita vya rushwa au vitisho yameweza kupenya na kuingia katika mfumo wa siasa, katika jeshi la polisi na hata katika vyombo vya mahakama vya Marekani na hivyo kuwa na ushawishi katika kupasishwa sheria ambazo zina maslahi kwao. Kwa kuzingatia hali hiyo, hata kama baadhi ya maafisa wa Marekani watakuwa na irada ya kweli ya kupambaa na matumizi na magendo ya madawa ya kulevya, lakini kuna vizingiti vingi mno katika njia ya kuweza kufikia lengo hilo.