SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 29 Machi 2016

T media news

Ajali za Mabasi zaendelea Kutumaliza...Hii Hapa Ajali Nyingine Iliyochukua Uhai wa Watu


Watu sita wamekufa na wengine zaidi ya 38 kujeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Iringa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Iringa kupinduka mlima Ipogolo Manispaa ya Iringa.


Mganga Mkuu Mkoa wa Iringa, Dk Robert Salim alisema waliokufa ni sita, wawili kati yao walifia hospitalini wakati wakipatiwa matibabu.


Dk Salim alisema waliokufa ni wanaume wanne na wanawake wawili na kwamba, maiti waliotambuliwa ni wawili, Makka Msigwa na Venant Mhagama.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 3.30 usiku baada ya basi la Lupondije aina ya Scania lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Iringa kumshinda dereva na kupinduka.


Alisema majeruhi 38 walifikishwa hospitalini hapo, 11 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 27 wamelazwa kwa matibabu.


Kakamba alisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.


Mmoja wa abiria walionusurika katika ajali hiyo, James John alisema walipofika Iringa, dereva waalikataa kuwashusha abiria waliokuwa wakiishia mjini ili awapeleke waliokuwa wakienda Mbeya kwenye basi jingine eneo la Ipogolo.


John alisema kutokana na uamuzi huo abiria waliotakiwa kushuka Kituo cha Kihesa na Kituo Kikuu cha Mabasi Iringa walipitiliza, lakini hawakufika Ipogolo wakapata ajali eneo la mlimani.


Dereva huyo, Castory Mwalusako (35) alisema basi hilo lilimshinda wakati akishuka mlima kutokana na kupoteza upepo kwenye breki na kulikwepa gari dogo lililokuwa mbele yake na kupoteza mwelekeo kisha kupinduka.