SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 6 Machi 2016

T media news

Ummy aagiza utumbuaji majipu idara ya afya


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amezipa meno taasisi za idara ya afya, wakuu wa mikoa na wilaya kuwashughulikia wahudumu wa afya watakaokwenda kinyume na maadili ya kazi zao.

Ummy aliziagiza taasisi hizo ikiwamo Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC), makatibu tawala na wakurugenzi kuchukua hatua zinazostahili.

Waziri huyo alitoa tamko hilo jana, ikiwa ni wiki moja tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutumbua majipu kadhaa katika Hospitali ya Ligula mkoani Mtwara na baadaye Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Hamis Kigwangalla kufanya hivyo katika Hospitali ya Temeke.

Ummy aliyaagiza mabaraza hayo kuwachukulia hatua na kuwafutia usajili na leseni zao wahusika iwapo watabainika kwenda kinyume na maadili ya kazi zao.

Katika tamko hilo, alisema wizara haitawavumilia watumishi wa sekta ya afya watakaokwenda kinyume na matakwa ya maadili ya taaluma zao katika vituo vya kutolea huduma.

“Katika utoaji wa huduma za afya yapo maadili ambayo mtoa huduma anapaswa kuyajua na kuyazingatia ikiwamo faragha, uaminifu, usawa, usiri na uhusiano,” alisema.

Pia, alisema mtoa huduma anatakiwa kumheshimu mgonjwa.
6