Makamu Chansela wa Ujerumani amesema Donald Trump, mgombea wa kiti cha rais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican ni hatari kwa amani na maendeleo duniani.Katika mahojiano na gazeti la Welt Am Sonntag, Sigmar Gabriel ambaye pia ni Waziri wa Uchumi wa Ujerumani amemfananisha Trump na Marine le Pen, mkuu wa chama cha mrengo wa kulia cha Ufaransa FN na Geert Wilders, kiongozi wa chama kingine cha mrengo wa kulia cha Uholanzi; ambao amesema wana misimamo mikali na hatari kwa usalama, amani, muamala wa kijamii na maendeleo ya dunia. Matamshi ya Makamu Chansela wa Ujerumani ni mwendelezo wa kauli za viongozi wa bara Ulaya ambao wameeleza wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa kuteuliwa Trump kuwa mgombea urais wa Marekani kupitia chama cha Republican.Hivi karibuni, Waingereza nusu milioni walisaini waraka unaoitaka serikali ya nchi hiyo kumzuia Donald Trump kuingia nchini humo baada ya kutoa wito wa kuzuiwa Waislamu kuingia Marekani.Vilevile mwanasiasa huyo mbaguzi aliwahi kutoa mwito wa kutumiwa mbinu za Manazi wa Ujerumani chini ya uongozi wa Adolph Hitler dhidi ya wafuasi wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu nchini Marekani.