SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 6 Machi 2016

T media news

MAULID MTULIA : Nitawaondoa Panya Road, wauza unga


Dar es Salaam. “Wilaya yetu ya Kinondoni inakabiliwa na janga la dawa za kulevya na vikundi vya vijana waporaji maarufu Panya Road. Inabidi tufanye jitihada kuwaokoa na hii ni moja kati ya vipaumbele vyangu.”

Ndivyo Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) alivyoanza kuzungumza na gazeti hili kuhusu maisha yake, familia na majukumu aliyo nayo katika jamii. Mtulia alishinda jimbo hilo kwa kupata kura 70,337 na kumuangusha mbunge wa zamani, Idd Azzan aliyeshika nafasi ya pili kwa kura 65,964.

Umaarufu wa mbunge huyo uliongezeka zaidi wakati wa sakata la bomoabomoa lililowakumba wakazi wa Mkwajuni, baada ya kuamua kufungua kesi ya kupinga nyumba za wananchi wake kubomolewa bila kuwapo kwa njia mbadala ikiwamo kupatiwa makazi mengine yenye usalama zaidi.

Anasema mkakati wake ni kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa kwenye halmashauri kupitia fedha zilizotengwa kwa ajili ya vijana.

Anatarajia kufanya kikao na vijana ‘walioshindikana’ kwenye jimbo lake wakiwemo wanaotumia dawa za kulevya na ‘Panya Road’ ili kuwafundisha maisha na kubadili fikra zao.

“Wapo vijana wanaonekana hawafai hata kidogo. Hawa wanahitaji matibabu maalumu. Nimepanga kukaa nao tuzungumze na kuona namna gani tunaweza kubadili mitazamo ili wawe na tija,” anasema.

Kwa makundi mengine kama bodaboda na wajasiriamali, anasema kuwa ameandaa mikutano kwa ajili ya kuwahamasisha wajiunge kwenye vikundi vya ujasiriamali ili mikopo itakapoanza kutolewa waweze kunufaika.

Akizungumzia maisha yake binafsi anasema: “Najivunia kuwa baba bora wa familia yangu na siyo bora baba, mke na wanangu wanayo nafasi ya pekee japo wanahitaji kunivumilia hasa kipindi hiki ambacho kazi na majukumu vimeongezeka. Uaminifu wangu kwao ni jambo la msingi zaidi,”

Upo usemi kwamba ndoa nyingi za watu maarufu wakiwamo viongozi na wasanii hazidumu na kama zitadumu, basi haziishiwi migogoro.

Mwenyewe anakiri kuwa nafasi yake na namna anavyozidi kuwa maarufu ndivyo majaribu yanavyoongezeka na kuhatarisha usalama wa familia yake.

Anasema heshima ya kiongozi huongezeka mara dufu anapoijali na kuitunza familia yake.

Alikotoka
Tangu akiwa mdogo alitamani siku moja aje kuwa kiongozi kwenye jamii inayomzunguka.

Anasema alipenda kusikiliza hotuba za viongozi mbalimbali na kwamba, aliyemvutia zaidi kwa wakati huo ni Mwalimu Julius Nyerere.

“CUF ni chama pekee nilichoamini kitaweza kutimiza ndoto zangu hivyo niliamua kujiunga nacho tangu nikiwa kijana mdogo. Nilijitahidi kushirikiana na wanachama wenzangu kuhakikisha tunafanya kazi kutimiza malengo ya chama,” anasema.

Kabla ya kuukwaa ubunge, Mtulia alikuwa mkuu wa idara ya elimu na dawa akisimamia shirika lisilo la kiserikali la ‘MDI’ linajihusisha na uendeshaji wa shule za msingi, sekondari na vyuo.

Anasema harakati za Uchaguzi Mkuu kupitia muungano wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), zilimuongezea nguvu ya kushinda nafasi hiyo kutokana na nguvu ya mabadiliko iliyokuwa ikitikisa. Anasema anaendelea kutekeleza ahadi zake na kuhakikisha anasimamia haki pamoja na kuwafichua wote wanavunja haki za binadamu.

Anataja baadhi ya vipaumbele alivyoanza kushughulikia kuwa ni pamoja na afya, elimu, uchumi, miundombinu, ajira kwa vijana, maji na huduma nyingine za kijamii.

Alivyovalianjuga bomoabomoa
Siku chache baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, sakata la kubomoa nyumba za watu waliojenga kwenye hifadhi za Mto Msimbazi liliibuka.

Mtulia anasema hatua ya wananchi wake kubomolewa bila kupewa taarifa wala fidia ilimfanya apate wazo la kufungua kesi ili kuwatetea.

“Niliamini sehemu pekee inakoweza kutendeka haki ni mahakamani, kimsingi lengo langu lilikuwa kusitisha ubomoaji ili watu wasikilizwe, walipwe haki zao ndiyo waondolewe,” anasema.

Anafafanua kuwa shauri lililofunguliwa Mahakama Kuu ni dogo linalofahamika kama ‘Miscellaneous land application’ namba 822 ya mwaka 2015. Hata hivyo, bomoabomoa ilisitishwa kutokana na ombi hilo ambalo bado linasubiri uamuzi wa mahakama.

Wito wake kwa wanaume
Anapinga ukatili wa kijinsia ambao baadhi ya wanaume wamekuwa wakiufanya dhidi ya wanawake.

“Wanaume wasisahau jukumu la malezi, wengi wametelekeza wake na watoto wao bila kujali maisha wanayokabiliana nayo, huu ni ukatili mkubwa ambao kwa pamoja lazima tuupige vita,” anasema. Anasema malezi ya watoto yanawahitaji wazazi wote wawili ambayo huwasaidia kujifunza mengi ikiwamo uongozi.

Anawashauri wanaume kujitahidi kutenga muda wa kukaa na familia zao hata kama wanayo majukumu mengi kwa madai kuwa, uongozi bora huanzia nyumbani.

“Utakuwaje kiongozi wakati familia yako imekushinda? Lakini pia watoto wetu wanajifunza uongozi kutoka kwetu akina baba. Usipotenga muda kwa ajili ya familia yako utakuwa unaidhulumu na jambo hilo sio jema hata kidogo,” anasisitiza.

Anawaambiaje wanawake
Anawataka wanawake kuwa wavumilivu kwa waume zao hasa wanapopitia kwenye kipindi kigumu ikiwamo kiuchumi au kimahusiano. Anasema marafiki wabaya na kusikiliza watu ndiko ambako kumekuwa kukisababisha ndoa nyingi kuvunjika na kuwaacha watoto wakihangaika.

“Ninamuomba mke wangu Fatuma Ngwale anivumilie. Pia, wanawake wengine wajue kwamba, kuna wakati tunahangaika kutimiza majukumu yetu ya kazi na siyo kila analosikia au hata kuliona linatafsiri ileile aliyonayo moyoni,”anasema.

Anawataka wasichana kufanya kazi kwa bidii, kwa madai kuwa huo ndiyo msingi wa maisha na mafanikio.

Anayemvutia katika siasa
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni miongoni mwa watu wanaomvutia kwenye ulingo wa kisiasa.

Anasema mara nyingi amekuwa akipenda kusikiliza hotuba za Mwalimu Nyerere ambazo humkumbusha kuweka suala la uzalendo mbele.

“Maalim Seif nimepata bahati ya kuwa naye na kuchota busara zake. Ninampenda ninatembea kwenye nyayo alizokanyaga. Sikuwahi kubahatika kuwa karibu na Mwalimu Nyerere lakini hotuba zake zinanifanya nihisi nipo karibu nae, najifunza mengi kupitia watu hao wawili,” anasema.

Ujasiri wake
Anasema ujasiri wake unatokana na kuwa kwake karibu na watu hususani wananchi wa jimbo lake.

“Ninapochanganyika na watu najiona nina ujasiri mkubwa kwa sababu bila wao, nisingekuwa na nafasi hii niliyo nayo. Siwezi kuacha kuwa nao karibu kwa kuwa ndio nguvu yangu,”anasema.

Udhaifu wake
Ameshindwa kupangilia muda. Mara nyingi amejikuta akifanya mambo mengi bila kumaliza kutokana na kushindwa kujua aanze na lipi na amalize na lipi wakati yote anaona ni ya muhimu.

“Kuna wakati nashangaa muda umeyoyoma na sijatimiza malengo ya siku hiyo, mambo yamekuwa mengi yananizonga na hakika nimeshindwa kabisa kuupangilia muda wangu. Huu ni udhaifu kwangu,” alisema.