Kujiunga Sudan Kusini na Jumuiya ya Afrika Mashariki
ukubwa wa hati Kichapishi Add new commentSudan Kusini imejiunga na Jumuiya ya Kieneo ya Afrika Mashariki (EAC).Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alitangaza habari ya kupatiwa uanachama Sudan Kusini katika Jumuiya ya EAC katika kikao cha jana cha viongozi wa nchi za jumuiya hiyo. Kikao cha Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilifanyika katika mji wa Arusha kaskazini mwa Tanzania.Shirika la habari la Ufaransa limeripoti kutoka Dar es Salaam Tanzania kwamba baada ya kujiunga Sudan Kusini, nchi wanachama wa EAC zimefikia sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Nchi hizo zina jamii ya watu karibu milioni 150.Jumuiya hiyo ya kieneo inajishughulisha na kuzihamasisha nchi wanachama kushirikiana katika masuala ya biashara na kurahisisha suala la ushuru wa mpakani kati ya nchi wanachama.Sudan Kusini mwezi Julai mwaka 2011 ilijitenga na Sudan na kujitangaza kuwa huru baada ya mapambano ya miaka kadhaa na serikali kuu ya Khartoum. Nchi hiyo mwezi Disemba mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kuibuka hitilafu kati ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na makamu wake, Riek Machar. Salva Kiir alidai kuwa baadhi ya wanajeshi katika jeshi la nchi hiyo wakiongozwa na Riek Machar walihusika na jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali yake.Pande hizo zilizokuwa katika mzozo huko Sudan Kusini hatimaye mwezi Agosti mwaka jana zilisaini makubaliano ya amani chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa ili kuhitimisha vita vya ndani vya umwagaji damu. Baada ya kupita muda na kuvunjika mazungumzo ya kusimamisha mapigano, Salva Kiir na Riek Machar mwezi Januari mwaka huu walifikia mapatano kwa minajili ya kugawana madaraka katika serikali ya mpito ya Sudan Kusini.Salva Kiir ambaye miaka mitatu iliyopita alimuuzulu umakamu wa rais Riek Machar kwa tuhuma kuwa alikula njama za kufanya mapinduzi dhidi yake, mwezi Februari mwaka huu alimrejesha tena katika wadhifa wake huo.Wakati huo huo Herve Ladsous, afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa hali ya mgororo wa kibinadamu nchini Sudan Kusini ni maafa na kwamba hali hiyo inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku. Ladsous ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kimataifa cha Kulinda amani huko Sudan Kusini amesema kuwa watu karibu elfu 50 wameuawa katika miaka miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Idadi hiyo ni mara tano ya ile iliyotangazwa na taasisi za masuala ya kibinadamu katika muda wa miezi mitano ya awali ya mgogoro wa Sudan Kusini.Herve Ladsous amesema kuwa watu karibu milioni mbili na laki mbili wamekuwa wakimbizi huko Sudan Kusini. Amesema raia hao wanakabiliwa na uhaba wa chakula.Wataalamu wa Umoja wa Mataifa mwezi Februari mwaka huu walizutuhumu pande zinazozozana huko Sudan Kusini kuwa zinawaua raia, kuwateka nyara na kupora mali zao. Licha ya kushuhudiwa lugha ya mapatano katika mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Salva Kiir na Riek Machar, lakini bado serikali ya mpito haijaundwa huko Sudan Kusini na hali ya kiuchumi na kibinadamu inatajwa kuwa ni ya maafa makubwa.Kamati ya Umoja wa Mataifa ambayo inasimamia usitishaji vita katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan Kusini, hivi karibuni iliwasilisha ripoti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya mambo ya nchi hiyo. Ripoti hiyo imefafanua kuwa, Salva Kiir na Riek Machar wangali wanadhibiti kikamilifu vikosi vya majeshi ya serikali na wanamgambo na kwa sababu hiyo wanahusika moja kwa moja na mauaji ya raia. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kinadhamini usalama na kuwalinda raia karibu laki mbili wa Sudan Kusini katika maeneo sita ya nchi hiyo. Pamoja na hayo yote mapigano katika mikoa ya Malakal na Wau yangali yanaendelea. Maafisa jeshi na wale wa serikali ya Sudan Kusini wanamtuhumu gavana wa mkoa wa Wau kuwa ndiye anayesababisha mgogoro na mivutano katika eneo hilo. Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika safari yake ya hivi karibuni huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini amewataka Rais Salva Kiir na Makamu wake, Riek Machar kutekeleza haraka iwezekanavyo vipengee vya makubaliano ya amani.
Maoni
Chapisha Maoni