SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 1 Machi 2016

T media news

Full Story Ujambazi wa Kivita

DAR ES SALAAM! Simulizi ya majambazi kuvamia Benki ya Access iliyopo Mbagala ya Rangi Tatu jijini Dar, Ijumaa iliyopita bado inasikika miongoni mwa jamii ikisema ilikuwa vita kamili huku masikitiko makubwa yakiwa kwa watu watano waliouawa ukiweka kando majambazi watatu ambao waliuawa na polisi.

 Hali ilivyokuwa baada ya tukio hilo la kutisha.
ALIANZA KUINGIA MWANAMKE
Hamis, mmoja wa majirani wa benki hiyo aliyekoswakoswa risasi, alisimulia alichokiona mwanzo hadi mwisho ambapo alikuwa na haya ya kusema:

 Wananchi wa Mbagala wakitaharuki baada ya tukio hilo.
“Ile ilikuwa ni vita kabisa! Ni vita jamani si ujambazi ule. Ilikuwa majira ya saa nane na nusu, nilimwona mwanamke mmoja akiingia benki. Huyu mwanamke nasikia ndiye alikuja kufanya ukaguzi wa mwisho. Alikuwa  kundi moja na majambazi.

 Gari lililopigwa risasi kwenye kioo chake.
“Hata hivyo, tuliambiwa kuwa baadhi ya wateja walimshtukia mwanamke huyo kwa sababu alipoingia, alisimama, akaangaza-angaza na kutoka. Wateja waliwaambia askari wa kampuni binafsi inayolinda hapa benki kwa kushirikiana na polisi wamhoji kwani aliashiria si mtu mzuri.

 

WENGINE WALIOUAWA KWA RISASI
Taarifa zinasema kuwa wengine waliouawa kwa kupigwa risasi na majambazi hao, ni kijana mmoja aliyekuwa akiuza vinywaji baridi pembeni ya benki hiyo, aliyekuwa akifahamika zaidi kwa jina la Mgosi. Inadaiwa kisa cha kupigwa risasi ni kitendo chake cha kupiga kelele akisema: ‘Wezi hao! Majambazi hao!’

 Wengine ni mama lishe aliyekuwa akienda kuchukua vyombo ndani. Yeye aliambiwa na majambazi hao akimbie lakini akasema: ‘Niende wapi wakati mimi nafuata vyombo vyangu?’

Pia kuna mwanamke mmoja yeye alikuwa akitoka ndani ya benki hiyo na kukumbana na majambazi.

 Naye mfanyakazi mmoja wa benki hiyo ambaye hakupenda kutaja jina lake, akisimulia sakata hilo, alisema:

“Ilikuwa vita! Mimi nilishangaa kuona kioo cha mlango kinamwagika chini sambamba na mlio wa risasi. Nikaona watu wameingia ndani wakiwa na bunduki. Ni tukio baya sana kulishuhudia.

 “Humu ndani walikwenda kujaribu kuvunja mlango wa chumba maalum cha kuhifadhia kiasi kikubwa cha fedha (strong room) lakini wakashindwa ndipo wakachukua zilizokuwepo kwenye droo nyingine. Kwa kweli hali ilikuwa mbaya sana, milio ya risasi ilitawala kila kona, watu tulikuwa tumelala kwa amri ya majambazi.

 “Walisema atakayepingana na amri yao watampiga risasi na kumuua. Sikumbuki hata kama nilikumbuka kusali kwa Mungu wangu.

POLISI WAFIKA
“Hata hivyo, haikuchukua muda  polisi wakafika na kupambana nao kwa kurushiana risasi. Gari la polisi lilishambuliwa kwa risasi. Unajua kilichotokea ni kwamba polisi wao walikuwa wakirusha risasi kwa tahadhari wasiwadhuru wananchi, majambazi  walikuwa wakizimimina kama mvua.”

 SHUHUDA WA NJE
Jerry Milo ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo, yeye alishuhudia vita yote mwanzo hadi mwisho. Alisema kuwa, jambazi mmoja aliyesimama barabarabni ndiye aliyekuwa na jukumu la kuzuia magari kupita eneo hilo.
Alisema: “Yule jambazi alikuwa na bunduki mbili. Alikuwa akifyatua risasi juu, nyingine upande wa magari. Alipoliona Defender la polisi akalifyatulia risasi, ikaingia kwenye kioo cha mbele lakini haikumpata mtu, Defender likaingia mtaroni.

MWANAJESHI ATAJWA
“Sasa hapo majambazi walishatoka benki na pesa. Wakaanza kukimbia wakiwa na bodaboda sita. Kila bodaboda walipanda wawili.

“Mwanajeshi mmoja wa JWTZ (Jeshi la Wananchi wa Tanzania) alitokea akiwa amevaa sare, akamfuata polisi mmoja, akamwonesha kitambulisho, akamwambia ampe bunduki, akapewa. Kazi ikawa kuwawahi wale majambazi maana walishaondoka na polisi wengine walikuwa wakiwafuata kwa nyuma.

BODABODA ROHO REHANI
“Suka (dereva) mmoja wa bodaboda aliyekuwa akipita maeneo hayo akienda Bunju baada ya kumpeleka mteja, alimuuliza yule mwanajeshi kama anaweza kupambana na majambazi hao apande pikipiki yake wawafukuze.

“Mjeshi akasema anaweza, akapanda. Alimwambia jamaa wa bodaboda kwamba akimgusa upande wa kulia alalie huko, akimgusa kushoto alalie hukohuko, nadhani ili apate nafasi ya kuelekeza mtutu wa bunduki mbele.”

MPAKA KIJIJI CHA CHURWI
Habari zinasema kuwa polisi kwa kushirikiana na mwanajeshi huyo waliwakimbiza majambazi hao mpaka kwenye Kijiji cha Churwi kilichopo Wilaya ya Mkuranga, Pwani ambako waliwaua watatu baada ya kurushiana risasi, tisa wakatokomea huku wakitelekeza pikipiki zao na bunduki tatu. Miongoni mwa waliouawa, mmoja alikutwa na hirizi shingoni.

KAULI YA KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Andrew Satta na kikosi chake wamekuwa katika oparesheni kali kwenye Pori la Mkuranga kwa siku zote na juzi aliliambia gazeti hili kuwa atahakikisha wahusika wote wanapatikana na kambi yao kusambaratishwa.

 WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ATOA TAMKO
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema amewasiliana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi ili apate ushirikiano kutoka JWTZ lililo chini ya mkuu wake, Jenerali Davis Mwamunyange ili kufanyike oparesheni ya nguvu katika misitu ya Mkoa wa Pwani ambako inaaminika kuna makundi ya majambazi.

Mwili wa marehemu Haridi ulisafirishwa Jumamosi iliyopita kwenda kwao Tanga kwa mazishi.

 SIMULIZI YA MAJIRANI WA BENKI

Baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka yaliyo jirani na benki hiyo ambapo walisimulia kile walichokiona.
“Sisi tulishtuka kusikia milio ya risasi. Ndipo tulipobaini kuwa ni majambazi. Walifunga barabara kwa kumimina risasi hovyo ambapo magari kutoka kusini na yale yaliyokuwa yakitoka Posta na Kariakoo yalishindwa kupita na hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akikatisha maeneo haya,” alisema jirani mmoja.

Hali ilivyokuwa ndani ya benki hiyo.
BUNDUKI NDANI YA MKEKA
“Lakini kabla hatua hizo hazijafanyika, ghafla nilimwona mwanaume mmoja amebeba mkeka wa China akiwa ameukunja.
“Alipokaribia, aliuweka chini mkeka huo na haraka sana akatoa bunduki moja aina ya SMG na kumfyatulia risasi polisi aliyekuwa na bunduki, Haridi Juma (28), kisha akarusha nyingine kwenye banda lao ambapo kulikuwa na polisi mwingine ambaye alijeruhiwa na akachukua bunduki zao.

WAONGEZEKA
Hali ya taharuki ilitokea,  ndipo nikaona majambazi wengine wakiongezeka na kuingia ndani ya benki sasa ambapo walimuua kwa risasi mlinzi wa kampuni binafsi.”