Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania kimekanusha taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amelazwa kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam.Akizungumzia chanzo cha kulazwa hospitali kiongozi huyo ambaye siku chache zilizopita alirejea nchini kutoka India aliokuwa matibabuni, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazrui amesema chanzo cha Maalim Seif kulazwa katika hospitali hiyo jana asubuhi ni uchovu wa safari yake ya India ambayo alienda kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.Mazrui amekanusha taarifa zilizokuwa zinaenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kiongozi huyo wa CUF alilazwa kutokana na matatizo ya moyo. Alisema kuwa hakuna kumbukumbu yoyote ya ripoti ya daktari inayoonesha kuwa Maalim Seif ana tatizo la moyo.Naibu Katibu Mkuu huyo wa CUF amesema kuwa kiongozi huyo anaendelea vizuri kiafya na kwamba hayuko katika hali mahututi kama ilivyokuwa ikielezwa.“Anakula na kufanya kila kitu mwenyewe na hata jioni hii nimeongea naye, anakula kila kitu, hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya afya ya Maalim Seif,” alisema Mazrui.Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa waliwasili katika hospitali hiyo kumjulia hali akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.../