SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 4 Machi 2016

T media news

Burundi yakaribisha kuteuliwa mpatanishi mpya mgogoro wa nchi hiyo

Burundi imeunga mkono kuteuliwa mpatanishi mpya kwa ajili ya kujaribu kutatua mgogoro wa nchi hiyo. Chama tawala cha CNDD-FDD jana Alkhamisi kilisema kuwa kuteuliwa Benjamin William Mkapa, rais wa zamani wa Tanzani akuwa mpatanishi mpya wa nchi hiyo ni hatua nzuri katika kuharakisha juhudi za kutatua mgogoro wa nchi hiyo.Pascal Nyabenda, mwenyekiti wa chama hicho amesema Mkapa ana wakati mwingi wa kuzungumza na mirengo pamoja na wananchi wa Burundi ili kuandaa mazingira ya kufikiwa matokeo mazuri ya kurejeshwa amani na uthabiti nchini Burundi. Kiongozi huyo wa Burundi amesema kuwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ataendelea kusalia katika nafasi yake ya kusaidia kuboresha mazingira ya mazungumzo ya Burundi lakini kwamba yeye peke yake hawezi kusimamia mazungumzo hayo. Katika kikao chao cha hivi karibuni viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walimteua Benjamin Mkapa kuwa mwenyekiti wa kundi la upatanishi wa mgogoro wa Burundi. Awali Museveni alikuwa ameteuliwa kuwa mpatanishi wa mgogoro huo. Licha ya kufanya vikao kadhaa vya mazungumzo na viongozi wa Burundi lakini rais huyo wa Uganda hakufanikiwa kupata matokeo yoyote ya kuridhisha. Baadhi ya wataalamu wa mambo walikosoa kuchaguliwa Museveni kuwa mpatanishi wa mgogoro huo, na hivyo tokea mwanzoni walikuwa wametabiri kufeli upataishi wake katika mgogoro huo.Wiki iliyo iliyopita, marais wa nchi tano za Afrika za Mauritania, Uganda, Senegal, Gabon na Waziri Mkuu wa Ethiopia wakiongozwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini waliitembelea Burundi na kutaka mazunguzmo ya haraka yafanyike ili kutatua mgogoro wa nchi hiyo. Hivi sasa kukubaliwa mpatanishi mpya wa mgogoro wa Burundi na viongozi wa serikali ya Bujimbura ni ishara nzuri kuwa viongozi hao wako tayari kuchukua hatua ya kutatuliwa kwa amani mgogoro huo ambao ulianza miezi kumi iliyopita kutokana na uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo wa kugombea tena urais kwa mara ya tatu mfululizo katika kile kilichoonekana na wengi kuwa ni kinyume na katiba ya nchi pamoja na mazungumzo ya amani ya Arusha Tanzania. Mivutano ya kisiasa na ghasia za ndani zimefikia hatua ambayo inaoonekana na wajuzi wa mambo kuwa zinaweza kuanzisha tena vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Ni kutokana na ukweli huo ndipo jamii ya kimataifa na hasa Umoja wa Afrika AU ukaanzisha juhudi kubwa katika siku za hivi karibuni kwa madhumuni ya kutatua kwa amani mgogoro wa nchi hiyo. Viongozi wa umoja huo wanasema kuwa vita vya aina hiyo huko Burundi vinaweza kuhatarisha usalama wa nchi nyingine za eneo hilo, na ndio maana wakasema kuwa hawataruhusu vita hivyo kutokea. Hata kama mazungumzo ya kutatua mgogoro wa Burundi hayajafanikiwa sana lakini kufuatia safari ya Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kisha ya viongozi kadhaa wa nchi za Kiafrika nchini humo, inaonekana kuwa mapatano ya kuhitimishwa mgogoro huo yamefikiwa kwa kiwango fulani. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba Burundi imekubali kutumwa nchini humo waangalizi wa kijeshi 100 wa Umoja wa Afrika na vilevile waangalizi 100 wa haki za binadamu. Awali Nkurunziza alikuwa amedai kuwa kutumwa nchini kwake waangalizi hao ni uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi hiyo.Wiki iliyopita, Léonce Ngendakumana mkuu wa chama cha upinzani cha Front for Democracy in Burundi alisema baada ya kukutana na ujumbe wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika kwamba wamekubaliana na suala la kuimarishwa upatanishi wa mgogoro wa nchi hiyo. Mgogoro huo hadi sasa umepelekea mamia ya watu kupoteza maisha na kujeruhiwa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi. Kutokana na juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kuumaliza, watu wa Burundi na jamii ya kimataifa ina matumaini kwamba mazungumzo ya amani yataanza hivi karibuni kwa shabaha ya kuhitimisha mgogoro huo wa kisiasa na hivyo kurejesha tena nchini humo usalama na utulivu wa kudumu.