Na Bashir Yakub.
Tunapoongelea upimaji ifahamike kuwa upimaji upo wa aina nyingi.Kutokana na hilo upimaji unaoongelewa hapa ni upimaji miliki. Lakini pia tunaongelea upimaji miliki wa ardhi mijini na sio vijijini. Upimaji wa ardhi miliki ni upimaji ambao lengo lake ni kummilikisha mtu ardhi.
Kummilikisha mtu ardhi sio kumuuzia ardhi. Kummilikisha mtu ardhi ni kutambua ardhi yake kimipaka na kumpatia nyaraka mahsusi(specific) inayohusiana na umiliki( hati).
Kwa maana hii wanaomiliki ardhi ambazo hazijapimwa hatuwezi kusema wamemilikishwa ardhi . Haijalishi ardhi hizo ni za kwao na wamezinunua kwa pesa zao. Kwa kusema hivyo haimaniishi kuwa ambao hawana hati au hawajapima ardhi zao basi sio wamiliki, hapana isipokuwa ni kuwa tu kwamba hawajamilikishwa kisheria na mamlaka za serikali.
Kutokana na hilo ardhi iliyopimwa na ile ambayo haikupimwa hutofautiana hadhi na thamani kwa kiasi kikubwa.
1.NYARAKA ZINAZOHITAJIKA ILI UPIMIWE ARDHI.
( a ) Barua kwenda kwa mkurugenzi. Anayetaka kupimiwa ardhi anatakiwa kuandika barua kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri husika. Barua ni nyaraka ya kwanza kabisa ambayo unatakiwa kuwa nayo. Ni katika barua hiyo ambamo utaeleza nia yako ya kutaka kupimiwa ardhi na matumizi ya ardhi yako kama ni makazi,kiwanda n.k.
( b ) Kuambatanisha mkataba wa mauziano. Katika hatua hii mkataba wa mauziano utatambuliwa kama nyaraka ya umiliki. Mkataba huu ndio utakaokutambulisha kama mmiliki wa ardhi husika. Huu unaambatanishwa kwasababu mmiliki wa ardhi ndiye mwenye jukumu la kuomba kupimiwa.
Hivyo kuambatanishwa kwa mkataba kunathibitisha kuwa mmiliki ndiye anayeomba kupimiwa kwa mujibu wa sheria. Ni vema mkataba wa umiliki ukawa ni ule mkataba wa kisheria ulioandaliwa na kushuhudiwa na mwanasheria.
( c ) Barua iliyotajwa hapo juu katika “A” hakikisha ina muhuri wa mwen yekiti wa serikali za mtaa, sahihi pamoja na mhuri wa mtendaji. Mwenyekiti na mtendaji atakayetumika sio wa pale unapoishi bali pale lilipo eneo unalotaka kupima. Kama eneo lipo unapoishi basi utamtumia huyohuyo wa eneo unaloishi.