SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu kipande cha video kinasambaa mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa Watanzania wanaoishi Oman wamekusanyika ofisi ya Ubalozi kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso na adhabu kali wanazopata kutoka kwa mabosi wao.
Imesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama kipande hicho cha video iliwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa madhumuni ya kujua usahihi wa jambo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo jana, Ubalozi ulitoa ufafanuzi kuwa uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi Oman na ulipangwa kufanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat Ijumaa.
“Matangazo ya mkutano huo yalitaka Watanzania watakaopenda kushiriki wajisajili kabla ya siku ya mkutano. Watanzania takriban 200 walijisajili na ubalozi ulifanya maandalizi ya ukumbi, vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu 300 kwenye hoteli ya Golden Tulip,” ilieleza na kuongeza:
“Siku ya mkutano ilipowadia, Watanzania zaidi ya 1,000 walijitokeza na kusababisha ugumu wa kuendelea na mkutano kutokana na maandalizi yaliyofanywa yalilenga watu 300.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati ya maandalizi ilipoona ukumbi umejaa na watu walio nje ni wengi mara mbili zaidi ya watu waliokuwamo ndani ya ukumbi, iliamua kufunga milango na kuwaomba waliochelewa warejee nyumbani.
“Uamuzi huo haukuwafurahisha watu waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe kwenye ukumbi wa mkutano, kitendo ambacho kiliashiria uwezekano wa kutokea vurugu kubwa.
Kutokana na uhalisia huo, Kamati ya maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi wa Watanzania wanaoishi nchini humo ilishauriana na kuamua kuwa mkutano huo uahirishwe na maandalizi yaanze upya kwa madhumuni ya kupata ukumbi na huduma nyingine zitakazokidhi idadi kubwa ya watu.”
“Wizara inapenda kuufahamisha umma wa kuwa kipande hicho cha video kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza kuingia kwenye ukumbi wa mkutano na sio kwamba wamekusanyika kwenye ofisi ya ubalozi wa Tanzania kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso wanayoyapata.”